Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini kwenda kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria Papa Francisko anawaalika waamini kwenda kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria 

Papa Francisko: Nendeni mkajifunze kutoka kwa B. Maria!

Katika shule ya Bikira Maria, waamini wanajifunza kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati; kwa njia ya Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, tarehe 12 Desemba 2018, imekuwa ni fursa ya kumwimbia tena Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa sababu ameutaza unyonge wa mjakazi wake, kwa maana, tazama tokea sasa vizazi vyote watamwita mbarikiwa! Ni kumbu kumbu endelevu ya ahadi ya Mungu kwa waja wake na mwaliko wa kuimba tena huruma na upendo wa Mungu kwa kurejea tena katika shule ya Bikira Maria. Huyu ni Mama wa Mungu na Kanisa anayewafundisha waamini sanaa ya utume na matumaini, kwa kutembea na kuimba!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Bikira Maria baada ya kupashwa habari kwamba, binamu yake Elizabeth alikuwa ni mjamzito, aliondoka kwa haraka kwenda kumsaidia. Ndivyo alivyofanya, alipowaona wanaharusi wa Kana ya Galilaya wakitindikiwa divai, akamwendea Yesu na kumhabarisha yale yaliyokuwa yanajiri.

Bikira Maria ni Mama aliyediriki kumsindikiza Mwanaye wa pekee katika hija ya maisha na utume wake, hadi akasimama chini ya Msalaba pale Mlimani Kalvari. Hivi ndivyo Bikira Maria alivyofanya pia kwa kumsindikiza Juan Diego, kiasi hata cha kuweza kupenya na kuingia katika maisha ya watu wa kawaida, ili kuwaonjesha wema na huruma ya Mungu, wale wote wanaoogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali kwa kuwafundisha kusimama imara katika imani na matumaini, hata pale mawimbi makali ya dhoruba yanapowajia.

Katika shule ya Bikira Maria, waamini wanajifunza kubaki imara katika safari, ili hatimaye, kuweza kufikia hatima yake, kwa kuwakirimia matumaini wale wote waliopokwa fadhila hii katika maisha! Hapa ni mahali pa kujifunza kuvumilia kwa imani na kuendelea kujikita katika mpango wa Mungu. Pamoja na Bikira Maria, waamini wanaendelea kutamadunisha na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kusimama kidete kulinda na kudumisha utakatifu wa maisha; kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kujenga na kuimarisha mshikamano; kwa kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili.

Katika shule ya Bikira Maria, waamini wanajifunza kutembea na kuimba matendo makuu ya Mungu katika maisha yao; ili kuwaonjesha furaha na matumaini wale waliokata tamaa na kumezwa na huzuni moyoni. Huu ni wimbo unaofumbatwa katika imani na matumaini, changamoto na mwaliko wa kujenga Hekalu lake takatifu, kama alivyofanya kwa Juan Diego, aliyewawezesha kuonesha sura zao na hivyo kuwa ni washiriki katika historia ya wokovu. Furaha ya Mwenyezi Mungu ni kuwaona watoto wake wakisimama kidete kulinda na kutunza mazingira; kwa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, hasa wale ambao wanateseka na kunyanyasika.

Katika shule ya Bikira Maria, waamini wanajifunza kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati; kwa njia ya Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Bikira Maria, waamini wanaendelea kujifunza kunyenyekea na kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika uchu wa mali, madaraka, umaarufu pamoja na kutaka kujikweza.

Kwa njia ya Bikira Maria, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake nguvu ya kuweza kupyaisha mshikamano, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi. Bikira Maria wa Guadalupe anakumbukwa na kuheshimiwa na familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini, ili kukuza na kudumisha uhai, ukarimu pamoja na kuwapatia nyenzo ya kujenga na kuimarisha Hekalu la Familia Takatifu ya Mungu. Bila wasi wasi wala makunyanzi, watu wa familia ya Mungu kutoka Amerika ya Kusini wanaweza kuimba na kutembea kama alivyofanya Bikira Maria katika maisha yake.

Papa: Kutembea na Kuimba
13 December 2018, 10:32