Vatican News
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Ufunuo wa umoja na upendo wa Mungu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Ufunuo wa umoja na upendo wa Mungu.   (Vatican Media)

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ufunuo wa umoja na upendo!

Tafuteni Uso wa Mungu aliye hai katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika umoja na upendo, changamoto na mwaliko kwa walimwengu kulitafakari kwa kina Fumbo la Utatu Mtakatifu ili kushinda kishawishi cha utengano duniani, kwa njia ya ushuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, watu wa Mungu waonje uwepo wake katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tafakari za Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2018  ni sehemu ya mchakato wa kutafuta Uso wa Mungu katika Maandiko Matakatifu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu”. Zab. 42:2. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujibidisha kuutafuta Uso wa Mungu aliyeumbwa mbingu na dunia, ili kuzama katika historia na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha, kama njia ya kupambana na changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Kipindi cha Majilio kisaidie jitihada za waamini kujenga mahusiano mema sanjari na kujiaminisha kwa Mungu, ili kuzama zaidi katika huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Kwa maneno machache, huu ni mwaliko wa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha ya kila siku, kielelezo cha mapambazuko ya imani. Mahubiri haya yanahudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Wakleri kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume walioko mjini Roma!

Padre Cantalamessa katika mahubiri yake ya Pili katika Kipindi cha Majilio, Ijumaa, tarehe 14 Desemba 2018, anasema ni mwaliko kwa waamini kuutafuta Uso wa Mungu aliye hai katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika umoja na upendo, changamoto na mwaliko kwa walimwengu kulitafakari kwa kina Fumbo la Utatu Mtakatifu ili kushinda kishawishi cha utengano duniani, kwa njia ya ushuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, watu wa Mungu waonje uwepo wake katika maisha yao!

Kwa mara ya kwanza, Musa alionja uwepo hai wa Mungu mbele ya macho yake katika kijiti kilichokuwa kinawaka moto bila kuteketea, akaonja ukuu, uzuri, wema na utakatifu wa Mungu unaofumbatwa katika kazi ya uumbaji, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchuchumilia hija ya utakatifu wa maisha, kwa kujikita katika upendo, kwani Mungu ni upendo! Mungu, Baba ni Nafsi ya kwanza katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani: Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayetakatifuza. Kanisa linaungama kwamba, kuna Mungu mmoja tu, kwa asili, kwa uwamo na kwa uwapo! Kumbe, Mwenyezi Mungu ni kielelezo cha upendo wa daima, ambao waamini wanaweza kuutafakari katika safari ya maisha yao!

Tafakari ya Mafundisho tanzu ya Kanisa juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu yanakazia ungamo la Umoja wa Uungu mmoja, yaani Mungu ni mmoja tu na wala hakuna mwingine. Iweni wamoja kama lilivyo Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo changamoto endelevu inayotolewa na Mama Kanisa, kama njia muafaka ya kuondokana na kishawishi cha utengano na mipasuko duniani! Jambo hili linawezekana ikiwa kama waamini watajikita katika tasaufi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na kuifanya kuwa ni sehemu muhimu ya maisha na utendaji wao wa kila siku! Hii ni tasaufi inayowakirimia furaha, wema na upatanisho unaowawajibisha kupendana, kwani Mungu ni upendo.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, “Nafsi na Asili” vinaonesha uwamo na uwapo mmoja kama anavyofafanua Mwinjili Yohane kwa kusema, “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki”. Huu ni mwaliko wa kuwa moyo mmoja na roho moja kama njia ya kumwilisha Amri ya upendo kutoka kwa Kristo, kielelezo cha ufunuo wa utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Watu wapendane, waheshimiane na kuthaminiana, daima wakitafuta: ustawi na mafao ya jirani zao. Jumuiya ipewe kipaumbele cha pekee dhidi ya ubinafsi na uchoyo kwa kuwa na moyo mmoja na roho moja ili kudumisha karama ya upendo katika umoja na utofauti.

Waamini katika kipindi hiki cha Majilio wanaalikwa kutafakari, kuiga na kuzama katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa njia ya maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, kwani kwa kumwona Kristo katika maumbo ya mkate na divai, waamini kwa jicho la imani, watamwona pia Mungu Baba na Roho Mtakatifu; tayari kumtolea ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji inayofumbatwa katika Fumbo la Kanisa. Haitoshi kusikia na kuona ili kulifahamu Kanisa.  Utatu Mtakatifu ni fumbo na kielelezo cha imani tendaji; mwaliko kwa waamini kuutafuta Uso wa Mungu aliye hai katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Utatu Mtakatifu
14 December 2018, 11:12