Tafuta

Vatican News
Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Tanzania Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Tanzania. 

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Tanzania!

Ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot Tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Antony Mayala aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania aligusia: Shukrani kwa wamisionari waliojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania sanjari na jubilei ya miaka 100 ya wakleri nchini Tanzania; kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Tanzania ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania. Baba Mtakatifu alifafanua kwamba, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Wamisionari wa Roho Mtakatifu wakafungua njia ya uinjilishaji kwa kuanzia Bagamoyo na kufuatiwa na Shirika la Wabenediktini pamoja na Wamisionari wa Afrika. Kutokana na juhudi, ari na moyo wao wa kujisadaka, Injili ya Kristo ikaenea kwa haraka sehemu mbali mbali za Tanzania na hivyo kujikita katika akili na nyoyo za watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuliwezesha Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kusherehekea Jubilei ya miaka 100 tangu lilipopata mapadre wake wazalendo. Hawa ni akina PadreAngelo Mwilabule, Celestin Kipanda, Ansgarius Kyakaraba pamoja na Wilbardi Mupapi. Katika orodha hii, Baba Mtakatifu anamkumbuka pia Kardinali Laurian Rugambwa, Kardinali wa kwanza Mwafrika, aliyeteuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII kunako mwaka 1960. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuiwezesha Tanzania na Vatican kufanya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu nchi hizi mbili zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, hapo tarehe 11 Aprili kwa ridhaa ya Mtakatifu Paulo VI. Nchi hizi mbili zimeendelea kudumisha urafiki kwa kuheshimiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili. Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa kwa kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Tanzania.

Ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot Tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Antony Mayala aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kuomba ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwa msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia familia ya Mungu nafasi ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhuru, siku moja tu, baada ya kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake mkuu wa mwaka uliofanyika Juni 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini  Tanzania ifikapo tarehe 9 Desemba. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika barua yake kwa ajili ya tukio hili anasema, uamuzi huu ni utekelezaji wa zawadi iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 kwa kuiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Kumbe, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania, Siku kuu ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili kitaifa nchini Tanzania iliadhimishwa rasmi tarehe 9 Desemba 2016. Hii ni nafasi ya kuombea familia ya Mungu nchini Tanzania ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, nguzo msingi ambazo daima zimewatambulisha watanzania katika Jumuiya ya Kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezesha watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Mtakatifu Yohane XXIII aliwaombea watanzania upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele!

B. Maria: Tanzania
08 December 2018, 15:56