Cerca

Vatican News
Tarehe 12 Desemba, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe. Tarehe 12 Desemba, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe  (Vatican Media)

Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Papa kuongoza Ibada!

Baba Mtakatifu Francisko ana Ibada ya pekee kwa Bikira Maria wa Guadalupe anayewaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kumwachia Mungu nafasi katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria. Hii ni Ibada kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu; haki na amani duniani, lakini kwa namna ya pekee huko Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 12 Desemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini. Kama ilivyo ada, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican ili kuomba ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria wa Guadalupe, hasa kwa familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini ambayo kwa sasa ina kabiliwa na changamoto nyingi.

Lengo ni kuombea mchakato wa uinjilishaji mpya miongoni mwa waamini wa Amerika ya Kusini; ili waweze kukua na kuimarika:kiimani na kiutu, daima wakijitahidi kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani, umoja na mshikamano wa dhati. Kwa namna ya pekee, maadhimisho haya ambayo ni moto wa kuotea mbali, yanafanyika nchini Mexico na maeneo ambayo Ibada kwa Mama Bikira Maria wa Guadalupe imeenea kwa kiasi kikubwa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ana Ibada ya pekee kwa Bikira Maria wa Guadalupe anayewaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kumwachia Mungu nafasi katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria. Hii ni Ibada kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu; haki na amani duniani, lakini kwa namna ya pekee huko Amerika ya Kusini. Ibada ya Misa itaanza saa 12: 00 kwa saa za Ulaya, lakini itatanguliwa kwa Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi.

Ni muda muafaka wa kuombea pia maadhimisho ya Siku ya thelathini na nne ya Vijana Duniani yatakayofanyika huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu.

B. Maria: Guadalupe
11 December 2018, 11:13