Baraza la Makardinali Washauri limehitimisha mkutano wake wa 27 Baraza la Makardinali Washauri limehitimisha mkutano wake wa 27 

Baraza la Makardinali Washauri lamaliza mkutano wake wa 27

Makardinali washauri wamewasilisha Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili. Makardinali wamepembua kazi yao katika kipindi cha miaka mitano; wameangalia muundo wake kwa kuzingatia kwamba, baadhi ya Makardinali umri unazidi kwenda mbio na kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa wanapaswa kung’atuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali Washauri limehitimisha mkutano wake wa 27, ulioanza tarehe 10-12 Desemba 2018 kwa ushiriki wa Makardinali wote isipokuwa Kardinali Pietro Parolin aliyekuwa na majukumu mengine ya kikazi nje ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko ameongoza mkutano huu, isipokuwa Jumatano asubuhi, kwani alipaswa kutoa katekesi kwa mahujaji na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Haya yamesemwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatano, tarehe 12 Desemba 2018. Makardinali washauri wamewasilisha Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili. Makardinali wamepembua kwa kina na mapana kazi ambayo wameifanya katika kipindi chote hiki cha miaka mitano; wameangalia muundo wake kwa kuzingatia kwamba, baadhi ya Makardinali umri unazidi kwenda mbio na kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa wanapaswa kung’atuka kutoka madarakani.

Baadhi yao tayari wamekwisha andika barua za kung’atuka na kupata ridhaa ya Baba Mtakatifu Francisko. Kati yao ni Kardinali George Pell, kardinali Francisco Javier Erràzuriz pamoja na Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Kwa sasa, Baba Mtakatifu Francisko hatarajii kuteuwa Makardinali wapya watakaoziba nafasi za wale wanaong’atuka. Mkutano huu umepembua pamoja na mambo mengine, kuhusu gharama ya uendeshaji wa shughuli za Vatican; Mkutano wa Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Baba Mtakatifu Francisko utakaofanyika kuanzia tarehe 21- 24 Februari 2019 ili kuangalia jinsi ambavyo Kanisa linaweza kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya kuwalinda watoto pamoja na Katiba ya Kitume kwa ajili ya Sekretarieti kuu ya Vatican.

Katika mkutano huu wa Makardinali washauri, wameshiriki pia Askofu Marco Mellino, Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Makardinali Washauri, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Oktoba 2018 na anatarajiwa kuwekwa wakfu kama Askofu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 15 Desemba 2018. Kardinali Reinhard Marx, Mratibu wa Baraza la Kipapa la Uchumi amedadavua mpango mkakati wa kubana matumizi kwa kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali ya Vatican. Hadi wakati huu, Vatican haina mpango wa kupunguza wafanyakazi wake, bali mkazo ni kuwa na mpango wa kazi; kuunganisha shughuli zinazolandana pamoja na kuwapatia uhuru wafanyakazi wanaotaka kustaafu mapema. Kwa sasa kuna mpango mkakati wa kubana matumizi kwa kipindi cha miaka mitano na wanaendelea kujielekeza kwa kuwa na mpango wa miaka kumi kuanzia sasa.

Makardinali wamedadavua pia mkutano wa Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani pamoja na Baba Mtakatifu Francisko; changamoto kwa Kanisa kusimama kidete kulinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, kashfa ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano amewaelezea Makardinali utekelezaji wa mageuzi kwenye Baraza lake kadiri ya Barua binafsi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ya mwaka 2015, kwa kuunganisha: Radio, Televisheni na Gazeti la L’Osservatore.

Lengo ni kuongeza tija ili kuleta ufanisi katika huduma kwa kuunganiha vyombo vya mawasiliano vya Vatican ambavyo vina utajiri mkubwa wa watu kutoka katika tamaduni na lugha. Professa Vinvenzo Bonomo, Gombera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano na mjumbe wa Serikali ya Vatican, amegusia sheria, taratibu na kanuni mpya za mji utawala wa mji wa Vatican zilizoridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 7 Desemba 2018. Baraza la Makardinali litakutana tena, kuanzia tarehe 18-20 Februari 2019.

Baraza Makardinali

 

 

13 December 2018, 10:44