Papa Francisko: Litakatifuzeni Kanisa kwa chachu ya utakatifu wa maisha! Papa Francisko: Litakatifuzeni Kanisa kwa chachu ya utakatifu wa maisha! 

Papa Francisko: Pyaisheni uso wa Kanisa kwa chachu ya utakatifu!

Kwa njia ya utakatifu wa maisha, Kanisa linaweza kupyaisha ari ya maisha ya kiroho na utume wake. Mafuta ya utakatifu yanaweza kulisaidia Kanisa kuganga na kutibu majeraha ya watoto wake na walimwengu katika ujumla wao, kwa kuonesha utimilifu wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C. PP. S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku Kuu ya Watakatifu Wote anasema, watakatifu wanawasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda wa Kristo na vyombo vya uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo! Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018, inasema, vijana wanalichangamotisha Kanisa kusimamia ukweli na uwazi, ili liweze kuwa mwanga angavu na chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika utakatifu wa maisha. Hii ni changamoto ya kuondokana na: ubaya wa dhambi, unafiki, kiburi, kinzani na migawanyiko isiyokuwa na tija wala mashiko, rushwa na kashfa ambazo zimepekenya na kuchafua maisha na utume wa Kanisa!

Kutokana na changamoto hizi, Kanisa halina budi kujikita katika toba na wongofu wa kimisionari tayari kuambata utakatifu wa maisha. Vijana wana ndoto ya kuona watakatifu wanaowafunda watakatifu wengine, kwani utakatifu ni sura pendevu ya Kanisa! Kwa hakika, vijana wanataka kusikia lugha ya utakatifu wa maisha ambao ni wito wa kwanza kwa kila mwamini kama wanavyokaza kusema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa njia ya Utakatifu wa maisha, Kanisa linaweza kupyaisha ari ya maisha ya kiroho na utume wake. Mafuta ya utakatifu yanaweza kulisaidia Kanisa kuganga na kutibu majeraha ya watoto wake na walimwengu katika ujumla wao, kwa kuonesha utimilifu wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12)  katika sura ya nne anapenda kukazia zaidi: udumifu, uvumilivu na unyenyekevu wa moyo kama alama za utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo dhidi ya tabia matumizi ya nguvu, ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya mtu kujiridhisha binafsi katika ufahari wake. Wakristo wawe wanyenyekevu kwa kujikita katika ukweli na uwazi; utu wema pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya ulimi!

Waamini wafurahie pia mafanikio ya jirani zao, wawasahihishe kwa upole na udugu pale wanapolegea katika dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa na huu ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo. Kuna waamini wanaoendelea kusimamia haki, amani na maridhiano katika jamii kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa wanahesabika kuwa ni vyombo vya amani! Maisha ya Kikristo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, furaha ya kweli inafumbatwa katika upendo!

Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na utulivu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha umoja na upendo wa kidugu. Waamini waoneshe uhuru na upendo wa ndani kabisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upya wa maisha yao! Familia ya Mungu ioneshe ujasiri wa kutoka kifua mbele kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa nyakati mbali mbali ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utakatifu ni hija inayofumbatwa pia katika maisha ya kijumuiya na Mama Kanisa anayo mifano kede kede ya Jumuiya za watakatifu. Hawa ndio akina Paul Miki na wenzake au Wamonaki waliouwawa hivi karibuni huko Algeria. Hawa ni watakatifu ambao wameishi kwa pamoja huku wakiadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kujenga umoja na udugu. Hawa ni kama Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali pa kurutubisha upendo, umoja na udugu; kwa kusaidiana na kutakatifuzana katika maisha, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, utakatifu unafumbatwa katika maisha ya sala kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kumbe, sala endelevu ni chachu ya utakatifu wa maisha! Ukimya na tafakuri  ni nyenzo zinazojenga uhusiano mwema na Kristo! Lakini, sala ya kweli inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yanayofumbatwa katika upendo. Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha kwani hiki ni kiini na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti za Kanisa, ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo!

Alama za Utakatifu
01 November 2018, 16:38