Ijumaa ya Huruma ya Mungu: Papa Francisko awatembelea wagonjwa na maskini wa Roma Ijumaa ya Huruma ya Mungu: Papa Francisko awatembelea wagonjwa na maskini wa Roma 

Siku ya Maskini Duniani: Papa Francisko awatembelea wagonjwa na maskini Roma!

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa ya Huruma ya Mungu, tarehe 16 Novemba 2018, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia”. Zab. 34: 6 ametembelea Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kujionea mwenyewe huduma ya tiba inayotolewa na Kanisa.

Na  Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, alijiwekea utaratibu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yake, dhamana ambayo anajitahidi kuiendeleza kila wakati anapopata fursa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia, kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu uliotoa nafasi kwa waamini kuonja tena huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka katika maisha yao!

Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya, unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Mwaka wa huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa ya Huruma ya Mungu, tarehe 16 Novemba 2018, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia”. Zab. 34: 6 ametembelea Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kujionea mwenyewe huduma ya tiba inayotolewa na wafanyakazi kutoka sekta ya afya ndani na nje ya Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2018.

Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusalimiana na kila mtu aliyekuwepo kwa huduma na matibabu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Injili ya upendo na huruma kwa watu wa Mungu. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya aliyeratibu tukio hili anasema, maskini na wahudumu wa afya wameguswa sana na uwepo wa Baba Mtakatifu kati yao kama faraja na mshikamano kwa watu wanaoteseka: kiroho na kimwili! Huu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaonesha jinsi ambavyo Injili ya upendo inavyoweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, chachu muhimu sana katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda!

Mababa wa Kanisa wanasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu! Dhana ya umaskini inajikita katika: utu na heshima ya binadamu; kanuni maadili na utu wema! Leo hii, maskini wana kiu na hamu ya kutaka kusikilizwa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Dr. Giustina Betti, mmoja wa madaktari wanaotoa huduma kwa maskini kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani anasema, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza, kwa kushiriki kikamilifu katika matendo ya huruma, kwa watu wanaosahaliwa kutokana na umaskini wao wa hali na kipato! Huduma ya vipimo, tiba na ushauri nasaha ilifunguliwa rasmi tarehe 12 Novemba 2018 na huduma hii imekuwa ikitolewa kwa wahitaji kwa muda wa saa 14 kwa siku!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja na Mwenyezi Mungu,  ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Mungu, ili kusikiliza kilio cha maskini kwa kuwaokoa na kuwajengea uwezo wa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya kijamii. Hata leo hii kuna maskini wanaojitambulisha kama akina: Bartimayo kipofu, aliyepaaza sauti yake, kiasi hata cha kumfikia Yesu, akamponya upofu wake, akapata kuona tena. Hata katika ulimwengu mamboleo bado kuna watu ambao hawana: fursa za ajira wala fedha ya kutosheleza mahitaji yao msingi na matokeo yake, wengi wao wanatumbukizwa kwenye utumwa mamboleo! Wote hawa bado wanayo matumaini ya mtu anayeweza kuwaambia !Jipe moyo; inuka, anakuita!

Papa: Ijumaa ya Huruma ya Mungu
17 November 2018, 08:42