Vatican News
Rais Alain Berset wa Shirikisho la Uswiss, tarehe 12 Novemba 2018 amekutana na Papa Francisko mjini Vatican. Rais Alain Berset wa Shirikisho la Uswiss, tarehe 12 Novemba 2018 amekutana na Papa Francisko mjini Vatican.  (ANSA)

Rais Alain Berset wa Uswiss akutana na Papa Francisko mjini Vatican

Baba Mtakatifu pamoja na Rais Alain Berset wamegusia pia mshikamano wa dhati kwenye Jumuiya ya Ulaya na katika masuala ya kimataifa, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika udugu, haki na amani; kwa kuzingatia itifaki na sheria za kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Alain Berset wa Shirikisho la Uswiss ambaye baadaye alipata fursa ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, wakati wa mazungumzo yao, wamegusia uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya waamini walei wanaotoa huduma ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, maarufu kama “Swiss guaards”. Viongozi hawa wawili wameridhishwa kwa uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizi mbili, wakiwa na matumaini kwamba, uhusiano huu utaendelea kuboreshwa na kuimarishwa kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu pamoja na Rais Alain Berset wamegusia pia mshikamano wa dhati kwenye Jumuiya ya Ulaya na katika masuala ya kimataifa, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika udugu, haki na amani; kwa kuzingatia itifaki na sheria za kimataifa.  Katika mwelekeo huu, Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamegusia: wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, vita na suluhu zake, rufuku ya silaha za kinyuklia pamoja na biashara haramu ya binadamu!

Rais wa Uswiss
13 November 2018, 15:35