Vatican News
Papa Francisko: Siku ya 105 ya Wakimbizi 2019 kuadhimishwa tarehe 29 Septemba 2019 Papa Francisko: Siku ya 105 ya Wakimbizi 2019 kuadhimishwa tarehe 29 Septemba 2019  (AFP or licensors)

Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, 29 Septemba 2019

Maadhimisho ya Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 yataadhimishwa tarehe 29 Septemba 2019 kutokana na sababu za kichungaji. Ufafanuzi huu umetolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia maombi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kuadhimisha Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, Jumapili ya mwisho ya Mwezi septemba badala ya Jumapili ya Pili ya Mwezi Septemba ya kila mwaka kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali. Kumbe, Maadhimisho ya Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 yataadhimishwa tarehe 29 Septemba 2019 kutokana na sababu za kichungaji. Ufafanuzi huu umetolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

 

Baba Mtakatifu anasema mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji kuwa ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Waamini wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kumtambua Kristo Yesu kati ya wakimbizi na wahamiaji wa nyati zote, ili kuweza kumfungulia malango ya maisha yao na kumkaribisha.

Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, chimbuko lake ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa zima.

Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa wa kwanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mikakati ya Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana.

Mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na sababu za kichungaji akaamua Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji iadhimishwe Jumapili ya Pili ya Mwezi Septemba na sasa ameridhia mambo ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia kwamba, Siku hii iadhimishwe Jumapili ya mwisho ya Mwezi Septemba na kumbe, kwa mwaka 2019, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji itaadhimishwa tarehe 29 Septemba. Mabaraza ya Maaskofu yanapewa angalisho, ili kuzingatia marekebisho haya yaliyoridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko kadiri ya Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Wakimbizi Septemba 2019
21 November 2018, 10:41