Mwenyeheri Teodoro Illera Del Olmo na wenzake 15 ni mashuhuda wa uvumilivu na msamaha, chachu ya Injili! Mwenyeheri Teodoro Illera Del Olmo na wenzake 15 ni mashuhuda wa uvumilivu na msamaha, chachu ya Injili! 

Wafiadini ni mashuhuda wa uvumilivu na msamaha, chachu ya Injili

Hata leo hii kuna Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuuwawa, kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa nao ni mashuhuda wa imani katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa lina mshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi na uwepo wa Mwenyeheri Teodoro Illera Del Olmo pamoja na wafiadini wenzake 15 waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kutokana na chuki za kidini “Odium fidei”. Hawa ni mashuhuda wa imani ambao hata upanga umeshindwa kuwatenganisha na upendo wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumkirimia maisha ya uzima wa milele!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Novemba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, Mashuhuda hawa wa imani, kati yao kuna: wakleri, watawa na waamini walei waliouwawa katika maeneo, nyakazi na mazingira tofauti kunako karne ya ishirini wakati wa vita na madhulumu dhidi ya Kanisa. Ni watawa wanaotoka katika Mashirika matatu tofauti ya kitawa, kila Shirika likiwa na karama na utume wake, lakini wote wamesadaka maisha ili kushuhudia: ujasiri, ile furaha ya Injili inayofumbatwa katika imani, wito na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Machoni pa watesi wao, walionekana kuwa wamekufa, lakini, wao wanatangaza ushindi mintarafu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Jumamosi, tarehe 10 Novemba 2018 Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Teodoro Illera Del Olmo pamoja na wafiadini wenzake 15 kuwa Wenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Jimbo kuu la Barcellona, Hispania. Anasema, wafiadini hawa walikuwa ni mashuhuda wa imani, waliosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu, uhuru, demokrasia ya kweli na maridhiano kati ya watu. Maisha yao yaliyomiminwa ardhini kama mbegu, yamezaa mbegu ya mvuto wa Injili kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, baada ya kuinulia Msalabani, akawavuta wengi kwenda kwa Baba yake wa mbinguni!

Kardinali Giovanni Angelo Becciu anakaza kusema, huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao katika mwanga wa Injili, ili kuwakirimia waamini ujasiri wa kuweza kujisadaka kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake, chemchemi ya furaha ya maisha ya uzima wa milele. Hata leo hii kuna Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuuwawa, kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa nao ni mashuhuda wa imani katika ulimwengu mamboleo.

Jambo la msingi kwa Wakristo ni kuendelea kushikamana na kufungamana katika misingi ya: haki, amani na upendo; umoja, udugu na mshikamano; toba, wongofu wa ndani na msamaha wa kweli, kielelezo makini cha moto wa imani. Wafiadini ni alama ya upendo dhidi ya: chuki na ubaguzi na ukosefu wa uhuru wa kuabudu na kidini. Wafiadini ni mashuhuda wa uvumilivu na msamaha kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu Msalabani na kwa njia ya damu yao, wanaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani!

Papa: Wenyeheri

 

12 November 2018, 08:09