Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Dumisheni haki na usawa, ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Papa Francisko: Dumisheni haki na usawa, ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji: Jengeni haki na usawa!

Jukwaa hili la Kijamii Kimataifa kwa Mwaka 2018 linaongozwa na kauli mbiu “Kuhama, Kupambana, Kujenga na Kubadilisha”. Jukwaa hili lilianzishwa kunako mwaka 2001 kwa lengo la kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayofumbatwa katika: haki, usawa na maendeleo; kwa kujikita katika utandawazi wa mshikamano

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ni changamoto changamani inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali duniani, kwa kusimama kidete kupambana na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Kuna mambo msingi yanayoapswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mbinu mkakati wa kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kuimarisha umoja, ushirikiano na majadiliano katika ukweli na uwazi, lakini zaidi kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi!

Huu ni muhtasari wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Jukwaa la VIII la Kijamii Kimataifa kuhusu Wahamiaji lililofunguliwa rasmi tarehe 2-4 Novemba 2018 huko nchini Mexico na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa wakiwemo: Kardinali Carlos Aguiar Retes, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mexico, Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Mexico pamoja na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu.

Jukwaa hili la Kijamii Kimataifa kwa Mwaka 2018 linaongozwa na kauli mbiu “Kuhama, Kupambana, Kujenga na Kubadilisha”. Jukwaa hili lilianzishwa kunako mwaka 2001 kwa lengo la kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayofumbatwa katika: haki, usawa na maendeleo; kwa kujikita katika utandawazi wa mshikamano. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utandawazi wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, janga kubwa katika ulimwengu mamboleo!

Ili kuweza kufikia hatua hii, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika jamii kwa kubomoa miundo mbinu inayoendelea kusababisha uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, haki inapewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuwapatia sauti wasiokuwa na sauti; na hawa ndio wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum; wanaodharirishwa, kunyanyaswa na kubezwa! Ni kundi la watu wanaonyonywa, wanaotendewa ukatili na kubezwa na watu mbali mbali hata katika ukimya wao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kulaani vitendo hivi viovu katika jamii, bali, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuibua mbinu mkakati, utakaosaidia kupata suluhu ya changamoto hii kwa wadau mbali mbali kuendelea kuwajibika barabara! Katika masuala ya wakimbizi na wahamiaji mageuzi  haya yanarutubishwa na mapambano ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi kutumia karama na mapaji yao kikamilifu ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayofumbatwa katika: haki, mshikamano pamoja na ushiriki mkamilifu wa wanajumuiya wote, ili kweli ndoto ya ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi iweze kukamilika.

Kati ya mada zilizopembuliwa tangu mwaka 2001 mintarafu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni pamoja na: wakimbizi katika ulimwengu mamboleo; haki msingi za binadamu, mipaka ya nchi, sera na mikakati ya kujihami kisiasa; ubepari, athari za mabadiliko ya tabianchi na sera za uhamiaji ndani ya nchi. Kutokana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mambo makuu mawili ushauri na majadiliano, ili kuweza kufikia mchakato wa uhamiaji salama, unaoratibiwa na kufuata sheria, kanuni na miongozo ya Jumuiya ya Kimataifa zinazofumbatwa katika misamihati ifuatayo: Kupokelewa, Kulindwa, Kuendelezwa na Kuhusishwa katika sera na mikakati ya jamii inayotoa hifadhi. Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, wanasiasa, jumuiya za kiraia na Kanisa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mapendekezo yaliyotolewa kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji kwa Mwaka 2018 yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia ari na moyo wa ushirikiano pamoja na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kuheshimu na kuthamini dhamana na wajibu wa kila mmoja wao! Baba Mtakatifu anapenda kuitia shime Jumuiya ya Kimataifa, vyama vya kiraia kuendelea kusaidia kuragibisha mapendekezo haya ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.  

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wote kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kujenga na kudumisha haki na usawa kwa watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa, ili wakimbizi na wahamiaji wasitumbukie katika makucha ya wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!

Papa:Wahamiaji Mexico
03 November 2018, 15:27