Papa Francisko anataika Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika amani na wala si katika vita! Papa Francisko anataika Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika amani na wala si katika vita! 

Papa Francisko: Wekezeni kwenye amani na wala si katika vita!

Papa Francisko, Jumapili, tarehe 11 Novemba 2018, amelikumbuka tukio hili la kihistoria, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kukataa katu katu kutumbukia katika utamaduni wa vita na badala yake, kutafuta njia muafaka za kuweza kutatua kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii kwa njia ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 11 Novemba 1918, Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ikakoma na watu zaidi ya milioni kumi na tano waliathirika vibaya sana! Papa Benedikto XV katika Waraka wake wa kitume “Quod Iam Diu” yaani “Kwa ajili ya Amani ijayo” uliochapishwa tarehe 1 Desemba 1918 alionesha furaha yake ya ndani na shukrani kwa Mwenyezi Mungu baada ya waamini kusali, ili kukomesha vita, ili kuanza mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, na hatimaye, amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Papa Benedikto XV akasema, Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia yalikuwa ni maafa “yasiyokuwa na mashiko”.

Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 11 Novemba 2018, amelikumbuka tukio hili la kihistoria, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kukataa katu katu kutumbukia katika utamaduni wa vita na badala yake, kutafuta njia muafaka za kuweza kutatua kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii kwa njia ya amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, walimwengu wameshindwa kujifunza kutokana na madhara ya vita. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kusali na kuwakumbuka wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wakati wa kuwekeza katika amani na wala si katika vita! Kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na maskini kama alivyofanya Mtakatifu Martin wa Tour, kielelezo cha ujenzi wa utamaduni wa amani duniani!

Waraka wa kitume “Quod Iam Diu” wa Mwaka 1918  ulilitikisa Kanisa, lakini Papa Benedikto XV akasimama kidete kulaani vita iliyokuwa ni chanzo kikuu cha maafa, mateso na mahangaiko ya binadamu! Mapigano haya kila siku yaliendelea kusababisha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia. Hata baada ya miaka mia moja, bado Kanisa linakaza kusema, “vita ni majanga yasiyokuwa na mashiko”, kuna umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili na sera makini za kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kudumisha Injili ya amani na mshikamano duniani!

Papa Benedikto XV aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa amani endelevu, inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Aliwataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mapigano na kuanza kujikita katika nguvu ya kimaadili; dhana ambayo inafumbatwa katika ushuhuda wa kinabii. Kwa wakati ule yaliyonekana kuwa ni maneno yasiyokuwa na nguvu! Lakini, baada ya miaka 100, maneno haya bado yanagusa akili na nyoyo za watu dhidi ya vita na madhara yake. Badala ya kuwekeza katika utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha duniani, rasilimali hii ingeweza kuwekezwa zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wengi.

Papa: Vita Kuu I ya Dunia

 

12 November 2018, 08:54