Cerca

Vatican News
Papa Francisko awataka wafanyabiashara Wakristo kuzingatia kanuni maadili, mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu! Papa Francisko awataka wafanyabiashara Wakristo kuzingatia kanuni maadili, mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Zingatieni kanuni maadili, utu na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu anawataka wafanyabiashara Wakristo kuwa waaminifu katika wito na utume wao, daima wakijitahidi kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hizi ni tunu ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa hasa katika kupanga sera na mikakati ya uwekezaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Biashara ni wito mtukuka unaopaswa kufumbatwa katika misingi ya maadili na utu wema mintarafu tunu msingi za nguvu kazi; mambo yanayojidhihirisha katika masuala ya uchumi na fedha kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa licha ya mabadiliko ya nyakati. Utandawazi umeathiri sana mchakato wa shughuli za kiuchumi, malengo na utekelezaji wake. Kumbe, ni wajibu wa wafanyabiashara wakristo kutafakari masuala haya kwa kina na mapana, ili kulinda na kudumisha ustawi, mafao ya wengi, maendeleo endelevu na fungamani kama njia muafaka ya mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washikiri wa Kongamano la Ishirini na Sita la Kimataifa la Wafanyabiashara Wakristo, UNIAPAC, lililokuwa na linafanyika mjini Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 22-24 Novemba 2018. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Bruno Marie Duffè, Katibu mkuu wa Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu wakati wa ufunguzi. Baba Mtakatifu anawataka wafanyabiashara Wakristo kuwa waaminifu katika wito na utume wao, daima wakijitahidi kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hizi ni tunu ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa hasa katika kupanga sera na mikakati ya uwekezaji! Tunu msingi za Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa ziwe ni nyenzo katika sera na mipango yao ya masuala ya biashara na uchumi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, binadamu na uwezo wake ni kama hazina ambayo imehifadhiwa katika vyombo vya udongo, kwani dhamana kuu ya uwezo inatoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kazi ya binadamu! Changamoto ni kuhakikisha kwamba, biashara inaendeshwa kwa misingi ya familia, ili kuboresha hali na mazingira ya kazi na hivyo wafanyakazi kujisikia kuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji; kwa kutumia vyema na kikamilifu talanta na uwezo wao kwa ajili ya ustawi, utu na heshima ya binadamu sanjari na kuheshimu mazingira badala ya kuyaharibu!

Sera na mikakati ya uchumi ifuate kanuni ya mafao ya wengi inayotoa mwelekeo wa uwajibikaji wa kisiasa katika masuala ya kibiashara, tafiti, teknolojia, huduma ya ubora ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika udugu na bidhaa kuwafikia watu wengi zaidi. Ukuaji wa mfumo wa uchumi unahitaji: maamuzi, mipango, mifumo na michakato maalum kwa ajili ya ugavi bora zaidi wa mapato, ubunifu wa vyanzo vya fursa za ajira na uendelezaji wa maskini. Mwelekeo huu wa shughuli za kiuchumi unaweza kusaidia kuibua mfumo mpya wa kisiasa na kiuchumi unaofumbata mafao ya wengi na maana kubwa zaidi ya maisha. Biashara ni wito wa kutukuka unaopaswa kuvaliwa njuga na wahusika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema,  kuna haja ya kuendelea kujikita katika kanuni maadili na tunu msingi za nguvu kazi ili kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika kuendeleza kazi ya Uumbaji, kwa kutangaza na kudumisha Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika haki, upendo wa kijamii sanjari na kuheshimu utu wa binadamu. Shughuli za kibiashara zinapaswa kuwa ni ushuhuda wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kukuza na kudumisha uwajibikaji, ili kila mtu aweze kutumia vyema karama na vipaji vyake, hali ambayo kimsingi, inahitaji wongofu na ushuhuda, kwa kumwachia Mwenyezi Mungu kuwaongoza ili waendelee kukuza na kukomaza mfumo wa kijamii.

Papa: Biashara ni wito

 

29 November 2018, 15:46