Tafuta

Vatican News
Papa Francisko awataka vijana wa "Scholas Occurrentes" nchini Argentina kukuza na kudumisha utambulisho na asili yao! Papa Francisko awataka vijana wa "Scholas Occurrentes" nchini Argentina kukuza na kudumisha utambulisho na asili yao! 

Papa Francisko: Dumisheni na kukuza utambulisho na asili yenu!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna hatari kubwa, pale watu wanapopoteza utambulisho wao, asili, mahali na historia na matokeo yake ni: kuanza kuwabeza wengine, wanaogeuka kuwa kama tishio na adui wa kufyekelea mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina, kwa sasa inaapania kuendelea kuwa mahali pa vijana kutambua na kushuhudia Injili ya maisha, kukuza elimu na kudumisha malezi bora kwa kujenga utamaduni wa watu tofauti kukutana na kusherekea zawadi ya uhai, kila mtu akiwa na utambulisho wake makini unaojionesha wazi, kwani maisha ni jambo zito. Utamaduni wa watu kukutana hauna budi kuwa makini kwani unapaswa kupata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mtu na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" huko Buenos Aires nchini Argentina, tarehe Mosi Novemba, 2018 amekazia zaidi umuhimu wa utambulisho na asili yake; pamoja na mchakato wa kulinda na kudumisha asili hii kwa ari na moyo mkuu. Vijana wanapaswa kujiuliza swali msingi wao ni akina nani? Ni nini maana ya maisha, swali ambalo wanapaswa kulijibu kwa utulivu na kuliachia nafasi. Majibu ya swali hili anasema Baba Mtakatifu kamwe hayawezi kutolewa kwa computer au kutengenezwa kwenye maabara.

Mwanadamu daima yuko safarini, anaendelea kukua na kukomaa katika mtindo wa maisha na historia yake kama mtu binafsi, kiini cha utambulisho wa mtu binafsi. Kila mtu ni shuhuda, mtunzi na msomaji wa maisha yake. Kila mtu ni sehemu ya ndoto ya Mungu kwake binafsi, changamoto ni kuendelea kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, kwa kulinda na kudumisha utambulisho fungamani wa maisha ya mtu binafsi na ukweli wa ndani! Hii ni changamoto ambayo inawaogofya watu wengi, kwani kila utambulisho una historia yake inayobubujika kutoka katika familia, jumuiya na nchi fulani. Utambulisho wa mtu daima unakwenda sanjari na mahali alikotoka na chanzo chake ni Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna hatari kubwa, pale watu wanapopoteza utambulisho wao, asili, mahali na historia na matokeo yake ni kuanza kuwabeza wengine, wanaogeuka kuwa kama tishio na adui wa kufyekelea mbali. Chembechembe za uadui zilizoanza kama moshi, zimegeuka na kuwa ni mto wa kuotea mbali! Kumbe, utambulisho wa mtu lisiwe ni jambo la kutisha au chanzo cha migogoro na kinzani au sababu ya kufutilia mbali tofauti msingi zilizopo, bali ni chombo na daraja ya kukutana na wengine, ili kukua na kukomaa, kwa kuendeleza kumbu kumbu hai kuhusu: mahali anapotoka mtu, utamaduni wa watu wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kukuza na kudumisha mchakato wa ukomavu kwa kutunza kumbu kumbu hai inayofumbatwa katika majadiliano ya mahali anapotoka mtu kwa kuwa na matumaini makubwa zaidi. Kwa njia hii, watu wataendelea kujitajirisha zaidi. Utambulisho unafumbatwa mahali anapotoka mtu, changamoto na mwaliko kwa wanafunzi kukuza na kudumisha utambulisho wa mahali wanapotoka, ili kuheshimiana, kuthaminiana na kuaminiana kwa dhati. Wanafunzi wawe wadadisi na watu wa kupenda kukuza: historia na tamaduni za familia zao; kwa kujikita katika majadiliano na wengine ili hatimaye, kudumisha umoja na udugu.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote walioshiriki katika kuandaa na hatimaye, kuwawezesha wanafunzi kukutana. Hawa ni wazazi na walezi pamoja na viongozi wa serikali waliowafungulia malango ili kuweza kushirikisha mang’amuzi haya bila kusahau jumuiya mbali mbali za watawa waliowafungulia malango ya maisha yao, ili kuweza kutajirishana. Baba Mtakatifu anawataka wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" huko nchini Argentina, kujisadaka na hivyo kutoa nafasi kwa maisha, ili kuandika ukurasa mpya.

Vijana wathubutu kushikamana na kufungamana na jirani zao licha ya tofauti zao za: utamaduni na lugha, bali wawe  na ujasiri wa kuthubutu kukutana na wengine, tayari kuwashirikisha utajiri wa maisha na kwamba, wataendelea bado kuwa kama walivyo! Hii ndiyo kazi ya kisanii wanayoweza kuitekeleza katika maisha. Mwishoni, anawaomba waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya sala!

Papa: Arentina

 

01 November 2018, 16:19