Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 100 ya Uhuru wa Poland: Anawaombea: Imani, matumaini, mapendo na uhuru wa kweli! Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 100 ya Uhuru wa Poland: Anawaombea: Imani, matumaini, mapendo na uhuru wa kweli!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 100 ya Uhuru wa Poland: Imani, matumaini, mapendo & uhuru!

Mtakatifu Yohane Paulo II, shuhuda wa wema na huruma ya Mungu katika karne hii, aendelee kuwaombea wananchi wa Poland: Imani, matumaini na mapendo, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na matumizi sahihi ya zawadi ya uhuru!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Kusitishwa kwa vita kuu ya Kwanza ya Dunia, ulikuwa ni mwanzo wa mapambazuko mapya kwa familia ya Mungu nchini Poand, kwa kuanza kuandika historia mpya ya uhuru wa nchi yao. Tarehe 11 Novemba 2018, Poland inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu ilipojipatia uhuru wake. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, kwa ajili ya maadhimisho haya aliomtumia Askofu mkuu Stanislaw Gadecki, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland anasema, anapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbuka na kuwaombea neema ya: imani, matumaini na upendo kwa familia ya Mungu nchini Poland, ili kukuza na kudumisha umoja wa kitaifa, amani na uhuru wa kweli!

Hii ni sehemu ya Sala ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyoitoa kunako mwaka 1998 wakati Poland ilipokua inaadhimisha kumbu kumbu ya uhuru wake ambao ni matunda ya sadaka kubwa iliyotolewa na wananchi wa Poland, kiasi hata cha kuchangia katika: historia, utamaduni na tasaufi ya watu wa Bara la Ulaya. Wananchi wa Poland walijitosa kimasomaso kutafuta uhuru, ustawi na mafao ya wengi, kiasi hata cha kuthubutu kusadaka maisha yao yaliyokuwa yanafumbatwa katika matumaini kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Bwana wa historia na maisha ya watu wa Mataifa.

Imani iliendelea kuwa ni chachu ya umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Poland, licha ya tofauti msingi zilizokuwa zinajitokeza, kiasi kwamba, wakawa tayari kuanza kujikita katika mchakato wa ujenzi na ulinzi wa mipaka ya nchi yao. Baba Mtakatifu Francisko, anaungana na Kanisa nchini Poland pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa sifa na shukrani kutokona na: nguvu, wema, neema na baraka zake kwa familia ya Mungu nchini Poland kwa kipindi cha miaka mia moja iliyopita!

Wananchi wa Poland wameendelea kuonesha matumaini katika uhuru wa kweli, licha ya matatizo na changamoto zilizojitokeza wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Poland ikajikuta ikiwa chini ya utawala wa Kinazi na Kikomunisti! Papa Francisko anasema, Sala ya Mtakatifu Yohane Paulo II, shuhuda wa wema na huruma ya Mungu katika karne hii, aendelee kuwaombea wananchi wa Poland: Imani, matumaini na mapendo, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na matumizi sahihi ya zawadi ya uhuru!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Poland kwa kuiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Poland, Mama wa Jasna Gora, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia amani, ustawi na maendeleo fungamani kwa sasa na kwa siku za mbeleni!

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 8 Novemba, akiwa ameshirikiana na Kardinali Stanislaw Rylko, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Poland ilipojipatia uhuru wake. Ibada hii iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Roma, imehudhuriwa pia na viongozi wa Ubalozi wa Poland, wakleri, watawa na waamini walei kutoka Poland wanaoishi hapa mjini Roma.

Papa: Poland 100 Yrs
10 November 2018, 16:01