Tafuta

Miaka 150 ya Uinjilishaji: Muda wa kujikita katika majiundo endelevu, upyaisho wa Kanisa na uzalendo wa Kikristo! Miaka 150 ya Uinjilishaji: Muda wa kujikita katika majiundo endelevu, upyaisho wa Kanisa na uzalendo wa Kikristo! 

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Majiundo, Upyaisho

Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu anasema, kwa sasa Kanisa linapaswa kuwekeza zaidi katika sera na mikakati ya majiundo endelevu kwa waamini walei, wakleri na watawa ili waweze kujenga na kudumisha urafiki wa kweli na Kristo pamoja na Kanisa lake, chachu muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika ujumbe aliomwandikia Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya aliyemteua kumwakilisha katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania yanayoongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji: furaha ya Injili”, Jumapili, tarehe 4 Novemba, 2018 anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wamisionari mbali mbali mbali waliojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania, kiasi kwamba, mwaka 2017, Kanisa likaweza kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre nchini Tanzania. Sherehe hizi zinakwenda sanjari na Jubilei ya Miaka 50 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu!

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Kanisa nchini Tanzania linapoadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji anasema, Kanisa limekuwa na kupanuka, sasa ni wakati wa kukuza na kudumisha majiundo endelevu kwa familia ya Mungu, ili kulipyaisha Kanisa kwa kujenga na kudumisha uzalendo unaofumbatwa katika Ukristo, chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani!

Jubilei ni wakati muafaka wa kumshukuru Mungu, kuomba msamaha kwa toba na wongofu wa ndani; tayari kujikita katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Mungu kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani. Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 150 iliyopita, imeongezeka maradufu, sanjari na kukua kwa uwajibikaji wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa sasa Kanisa linapaswa kuwekeza zaidi katika sera na mikakati ya majiundo endelevu kwa waamini walei, wakleri na watawa ili waweze kujenga na kudumisha urafiki wa kweli na Kristo pamoja na Kanisa lake, chachu muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

 

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anakaza kusema, ujenzi wa Ufalme wa Mungu unapaswa kuanzia katika familia, Kanisa dogo la nyumbani; kwa kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, chombo bora cha tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali ambapo imani inashuhudiwa katika matendo: kiroho na kimwili. Ujenzi wa Kanisa watu, kiwe ni kipaumbele cha kwanza kwa Tanzania, baada ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji.

Mkazo zaidi uwe ni ushiriki mkamilifu na endelevu  wa waamini katika kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wahamasishwe zaidi na zaidi kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; kwa kujikita katika Katekesi makini na endelevu; kwa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kanisa kama nyenzo muhimu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili ya Kristo. Ongezeko la idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania liende sanjari na ubora wa maisha yao: kiroho na kimwili, ili waweze kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya familia ya Mungu inayowajibikiana!

Majiundo endelevu na fungamani ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuwajengea uwezo waamini kukabiliana na changamoto mamboleo, ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa katika: imani, matumaini na mapendo, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni rafiki na mwandani wa maisha yao. Kwa njia hii, waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati yao na kati yao na Mwenyezi Mungu asili ya wema, uzuri na utakatifu wa maisha. Haya ndiyo mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa!

Lengo kuu ni kuyatakatifuza malimwengu, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kumbe, cheche za mwanga wa Injili ya Kristo zinapaswa kupenya na kugota katika akili na nyoyo za watu: kisiasa, kiuchumi, kimaadili, kijamii na kiutu, ili uwepo endelevu wa Mungu na utendaji wake wa kazi uweze kudhihirika zaidi! Kwa njia hii, Kanisa litaweza kujipyaisha kwa kujikita katika tunu msingi za Injili na imani kwa Kristo Yesu.

Miundombinu sanjari na mihimili ya uinjilishaji nchini Tanzania imeongezeka maradufu, kwani leo hii Kanisa la Tanzania anasema, Askofu mkuu mstaafu Lebulu lina majimbo 34 yanayoongozwa na kuhudumiwa na Maaskofu wazalendo. Tanzania ingeweza kuwa na majiumbo mengi zaidi kama sehemu ya mkakati wa kupeleka huduma ya shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu, lakini bado kuna changamoto pevu kama rasilimali fedha, watu na vitu vinavyohitakika ili kuendesha jimbo kikamilifu.

Ongezeko la majimbo na Maaskofu wazalendo, iwe ni fursa kuambata na kujikita katika uzalendo unaofumbatwa katika Kristo, yaani: uongozi kwa Kanisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu. Huu ni uzalendo unaovuka mipaka ya utaifa, umajimbo, ukabila au mahali anapotoka mtu! Jambo la msingi ni umoja na udugu katika Kristo Yesu, aliyevunjilia mbali kuta zote za utengano kwa njia ya Fumbo la Msalaba, ili kujenga: Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Uzalendo wa kidugu miongoni mwa Wakristo unafumbatwa katika mchakato wa kuyatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha anahitimisha mahijiaono haya maalum na Vatican News kwa kusema, uzalendo una madai na majukumu makubwa, kwani unafumbatwa katika misingi ya kitume!

Jubilei 150 Tanzania
03 November 2018, 15:44