Tafuta

Papa Francisko asema, Jeuri ya vijana inafumbatwa katika huduma! Papa Francisko asema, Jeuri ya vijana inafumbatwa katika huduma! 

Papa Francisko: Siku ya XXXIV Vijana Duniani: Jeuri ya vijana inafumbatwa katika huduma!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa kizazi kipya wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama anawakumbusha kwamba, mapinduzi ya huduma ndiyo nguvu ya vijana wa kizazi kipya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

 

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa na Serikali ya Panama pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini humo wa kutembelea Panama kuanzia tarehe 23 Januari 2019 hadi tarehe 27 Januari 2019 ili kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo na tayari ratiba elekezi imekwisha kutolewa na Vatican.

Mama Kanisa katika kipindi cha mwaka 2018-2019 anapenda kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana, ili kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza kufanya maamuzi mazito katika maisha. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018 wanayataka Makanisa mahalia kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maana ya maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa kizazi kipya wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama anawakumbusha kwamba, mapinduzi ya huduma ndiyo nguvu ya vijana wa kizazi kipya! Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyediriki kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Huu ni ushuhuda wa ujasiri na ukarimu kwa mwamini aliyetambua siri ya wito wake, tayari kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, kuna umati mkubwa wa vijana mara baada ya kuhitimu masomo yake, unajisikia ndani mwake kuwa na mvuto unaowasukuma kuwasaidia jirani zao, hasa wale wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Mapinduzi ya huduma ndiyo chachu inayoweza kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu mamboleo, kiasi cha “kuwabwaga chini wenye nguvu”. Hii ni changamoto ya kujisadaka katika maisha, kwa kuendelea kujiaminisha, kujadiliana na kusikiliza kwa makini kama alivyofanya Bikira Maria, aliyesikiliza kwa makini ujumbe wa Malaika Gabrieli na hatimaye, kutoa jibu muafaka.

Uhusiano kati ya Bikira Maria na Mwenyezi Mungu katika ukimya unaofumbatwa ndani ya moyo, unaweza kuwasaidia vijana kung’amua miito yao ambayo inaweza kuwa ni katika maisha ya ndoa na familia; wito wa upadre na maisha ya kuwekwa wakfu; zote hizi ni njia za kumfuasa Kristo Yesu, jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa kuthubu kusema, “Mimi hapa Bwana”! Bikira Maria ni kati ya wanawake waliobahatika kuwa na furaha katika maisha, kwani alionesha ukarimu wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kukubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.

Mwenyezi Mungu hapendi kuzima matamanio halali na ndoto za vijana wa kizazi kipya, bali anataka kuzikuza na kuzikomaza, ili ziweze kuzaa matunda ya furaha na utulivu wa ndani. Kumpatia Mungu jibu la uhakika ni mwanzo wa chemchemi ya furaha inayosambaa na kuwafikia watu wengine. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuzama katika undani wa maisha yao na kumhoji Mwenyezi Mungu kile ambacho anataka kutoka katika maisha yao! Vijana wasiwe na haraka ya kutaka kupata majibu, bali wamwachie nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wao na hivyo wataweza kung’amua mabadiliko makubwa katika maisha yao na hivyo kuwaletea furaha.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, kwa kufuata na kutekeleza sera na mikakati waliyowekewa mbele yao, ili kufikia lengo la maadhimisho haya! Katika hija hii, kuelekea Panama, vijana wakumbuke kwamba, wanaongozwa na kusindikizwa kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kwa njia ya mfano wa maisha yake, anawahamasisha vijana kuwa na ujasiri na wakarimu, ili kutoa majibu yanayolainisha sakafu ya moyo!

Papa: Vijana Panama
22 November 2018, 14:07