Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 20019 Panama: ratiba elekezi ya Hija ya Kitume ya Papa Francisko! Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 20019 Panama: ratiba elekezi ya Hija ya Kitume ya Papa Francisko! 

Papa Francisko: Siku ya XXXIV Vijana Duniani 2019: Ratiba elekezi

Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya katika imani na udugu.

Ratiba elekezi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama inaonesha kwamba, Papa ataondoka Roma, Jumatano tarehe 23 Januari 2019 asubuhi na kuwasili majira ya jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Tocumen nchini Panama. Baba Mtakatifu atakaribishwa rasmi na viongozi wa Serikali na Kanisa na baadaye ataelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Panama kwa mapumziko.

Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu atamtembelea rasmi Rais wa Panama, Ikulu baadaye atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na wawakilishi mbali mbali wa vyama vya kiraia nchini Panama kwenye Jengo la Wizara la Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Panama. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kati, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assis na jioni, itakuwa ni patashika nguo kuchanika, kwani Baba Mtakatifu atafungua rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 katika uwanja Cinta Costera.

Ijumaa tarehe 25 Januari 2019, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Upatanisho kwenye Gereza la Vijana Watukutu. Atarejea kwenye Ubalozi wa Vatican kwa mapumziko mafupi na jioni ataongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kwa vijana na kutoa mahubiri. Jumamosi, tarehe 26 Januari 2019, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kubariki Altare ya Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Antiqua. Ibada hii itakuwa ni kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini wa vyama na mashirika ya kazi za kitume nchini Panama. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana pamoja na vijana kwenye Seminari kuu ya San Josè na jioni atashiriki katika Mkesha wa Sala kwa ajili ya kufunga rasmi Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Jumapili, tarehe 27 Januari 2019: Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na vijana kwenye Uwanja wa Yohane Paulo II; atatembelea Nyumba ya Msamaria Mwema kwa ajili ya Watoto Yatima na baadaye jioni, ataagwa na kufunga vilago kurejea mjini Vatican ili kuendelea na utume wake.  Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwasili mjini Roma Jumatatu tarehe 28 Januari 2019 majira ya asubuhi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Panama, tayari limebainisha maeneo makuu yatakayotumika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019, ambayo kimsingi, ni sehemu ya mbinu mkakati wa Mama Kanisa, katika mchakato wa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko sanjari na kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018, imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka.

Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

Papa: Panama
21 November 2018, 11:45