Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya II ya Maskini Duniani 2018: Kilio, Kujibu na Kukoa! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya II ya Maskini Duniani 2018: Kilio, Kujibu na Kukoa! 

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO KWA SIKU YA MASKINI DUNIANI 2018

Kilio cha Mzaburi ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangiko pamoja na mateso mbali mbali ya watu wanaojulikana kwa ujumla kama “maskini”. Huu ni mwaliko wa kuwaangalia, kuwasikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha mahangaiko yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Siku hii kwa mwaka 2018 inaadhimishwa Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa ambayo kwa Mwaka huu itakuwa ni tarehe 18 Novemba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia”. Zab. 34: 6 (Katika Biblia ya Kiswahili). Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Pili ya Maskini Duniani kwa mwaka 2018 anakazia mambo makuu matatu: Kilio, Kujibu na Kuokoa.

Kilio cha Mzaburi ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangiko pamoja na mateso mbali mbali ya watu wanaojulikana kwa ujumla kama “maskini”. Huu ni mwaliko wa kuwaangalia, kuwasikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha mahangaiko yao! Mwenyezi Mungu ni mwema na mwingi wa huruma kwa wale wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake kwa moyo uliovunjika na kupondeka; wale wanaoteseka kutokana na upweke pamoja na kutengwa na jamii. Anawasikiliza wale wote ambao wanyanyaswa katika utu na heshima, lakini bado wanaujasiri wa kuinua uso wao, tayari kupokea mwanga na faraja!

Mwenyezi Mungu anawasikiliza wale wote wanaodhulumiwa kutokana na ukosefu wa haki, sera na itikadi zinazokinzana na haki; watu wanaoogopeshwa kutokana na vita, lakini bado wanatambua kwamba, wanaye Mwenyezi Mungu ambaye ni Mkombozi wao. Kiini cha sala hii ya Zaburi ni ile hali ya mtu kujiachilia kwa kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu anayesikiliza na kuwakirimia waja wake. Kwa muhtasari Kristo Yesu katika Heri za Mlimani anasema, “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao”.  Mzaburi anasukumwa kutoka katika undani wa moyo mwake na ile hamu ya kutaka kushirikisha wengine, kwanza kabisa kama Mzaburi: maskini, watu waliotengwa na kukataliwa na jamii. Lakini hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na upendo wa Baba Mwenye huruma, hususan katika ulimwengu mamboleo ambamo utajiri unapewa kipaumbele cha kwanza, kiasi cha kuwafanya watu kujifungia katika ubinafsi wao.

Mzaburi anapoelezea uhusiano wake na Mwenyezi Mungu anatumia neno “Kilio”, hiki ni kilio kinachopasua mawimbi hadi kumfikia Mwenyezi Mungu huko mbinguni. Ni kilio kinachofumbata: mateso, upweke, hali ya kukata tamaa na matumaini, kiasi hata cha kushindwa kutua katika masikio ya binadamu? Anauliza Baba Mtakatifu Francisko kwa mshangano mkubwa! Hiki ni kilio kinachotua kwa watu wasiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ni muda wa kuchunguza dhamiri  na kuangalia ikiwa kama kweli wanadamu wanao uwezo wa kusikiliza kilio cha maskini!

Kuna haja ya kujenga ukimya anasema Baba Mtakatifu ili kutambua kilio cha maskini na kukukipatia majibu muafaka na wala si kwa ajili ya wahusika kutaka kujinufaisha wenyewe; bali kuwawezesha maskini kupata msaada. Huu ni utamaduni unaowafanya watu kujiangalia na kujitunza wenyewe, bila hata ya kuguswa na mahangako ya jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, neno la pili ni “Kujibu”: Mzaburi anasema, Mwenyezi Mungu anasikiliza na kujibu kilio cha maskini. Hili ni jibu linalofumbatwa katika historia ya ukombozi tangu kwa Mzee Abrahamu Baba wa imani, Mtumishi wa Mungu Musa ambaye Mwenyezi Mungu alijifunua jina lake kwake katika kichaka cha moto, akampatia utume wa kuwakomboa watu wake kutoka utumwani Misri. Wakatembea kwa muda wa miaka arobaini jangwani; wakaonja kiu na njaa; wakateleza na kuanguka majaribuni kwa kushindwa kuwa waaminifu kwa Agano na Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuabudu miungu wengine.

Mwenyezi Mungu akajibu kilio cha watu wake kwa kuwapatia wokovu, ili kuganga na kuponya madonda ya roho na mwili; kwa kuwajalia haki na kuwarejeshea utu na heshima yao. Hii ndiyo changamoto inayoweza kutekelezwa hata katika maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani inayopania kuliwezesha Kanisa walau katika hali na mazingira yake, kuweza kujibu kilio cha maskini wa kila aina, ili waweze kutambua kwamba, kilio chao kimejibiwa na wala hakikuangukia kwenye “masikio yaliyowekwa nta”. Inawezekana kwamba, jibu la Kanisa likawa ni sawa na “tone la maji baharani”, lakini ni alama muhimu sana ya mshikamano na uwepo endelevu wa ndugu katika mahangaiko! Watu washikamane na kujihusisha na wale wote wanaosikiliza kilio cha maskini duniani na kuwaonjesha upendo wa dhati; kwa kuwaheshimu na kusumbukia mafao yao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, neno la tatu ni ”Kuokoa” kwani maskini katika Biblia anauhakika kwamba Mwenyezi Mungu ataweza kuingilia kati na kumrejeshea utu na heshima yake. Umaskini ni matunda ya ubinafsi, kiburi, chuki na uhasama pamoja na ukosefu wa haki. Hizi ni dhambi za zamani kabisa katika maisha ya mwanadamu zinazowakumba hata watu wasiokuwa na hatia. Mwenyezi Mungu anakuja kuvunjilia mbali minyororo ya umaskini wa watu wake, kwa kusikiliza na kujibu kilio chao. Maskini watafurahia na kushangilia fadhili za Mungu kwa kuwa ameyaona mateso yao na kuwakoa na mtego wa wawindaji. Mwenyezi Mungu anawapokea watu wake, anawaonjesha urafiki.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kuungana pamoja na Mwenyezi Mungu, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Mungu ili kusikiliza kilio cha maskini kwa kuwaokoa na kuwajengea uwezo wa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya kijamii. Hata leo hii kuna maskini wanaojitambulisha kama akina: Bartimayo kipofu, aliyepaaza sauti yake, kiasi hata cha kumfikia Yesu, akamponya upofu wake, akapata kuona tena. Hata leo hii pia kuna watu ambao hawana: fursa za ajira wala fedha ya kutosheleza mahitaji yao msingi na matokeo yake, wengi wao wanatumbukizwa kwenye utumwa mamboleo! Wote hawa bado wanayo matumaini ya mtu anayeweza kuwaambia !Jipe moyo; inuka, anakuita!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wanaposikia sauti ya maskini, wanawajengea hofu; kwa “kuwapaka matope na kuwaambia watu kwamba, hawa ni watu hatari” kwa usalama, amani na utulivu nchi, kiasi cha kuwasukumia mbali, ili waweze kutokomea kiasi cha kusahau kwamba, kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anawapokea na kuwafariji kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kwa njia hii, dhambi inasamehewa na haki inashika mkondo wake na wote kwa pamoja na wanapaaza kilio chao na Mwenyezi Mungu atakuwa tayari kuwajibu! Mimi hapa!

Kwa kawaida maskini ni watu wa kwanza kuonja na kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao, kiasi hata cha kuweza kutolea ushuhuda wa maisha yao, hata nyakati za giza na usiku mnene, daima atawakirimia upendo na faraja yake. Lakini, ili kuweza kupata ukombozi wa kweli, kuna haja ya kuwepo na watu ambao  wataweza kujisadaka kuwasikiliza, kwa kuwafungulia malango ya nyoyo na maisha yao, ili kuwawezesha kujisikia kuwa ni marafiki, ndugu na jamaa. Kwa njia hii watawaweza kuonja nguvu inayokoa na kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kumwilisha kwa matendo maneno ya Mzaburi kwamba, maskini watakula na kusaza. Maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2017 yalipambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Maskini sehemu mbali mbali za dunia, waliweza kuonja wema, huruma, upendo, furaha, ukarimu, mshikamano na udugu. Haya ni mang’amuzi yanayowarejesha waamini kwenye ile Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, waliokuwa wakidumu katika fundisho la Mitume, katika ushirika na katika kuumega mkate; wakagawana mali zao kadiri ya mahitaji ya kila mmoja wao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, changamoto ya baa la umaskini ni kubwa sana duniani, inahitaji umoja na mshikamano, ili kuweza kuwapeleka watu wote kwa Mwenyezi Mungu na katika utakatifu. Hii ni changamoto inayofumbatwa katika imani na kutekelezwa katika mapendo; majadiliano na unyenyekevu katika mang’amuzi na ushirikiano katika utekelezaji wa changamoto hii mintarafu Injili. Mwenyezi Mungu ndiye anayechukua hatua ya kwanza kuwasaidia maskini! Kumbe, wadau wakuu ni Mwenyezi Mungu pamoja na maskini na kwamba, wasamaria wema wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anasema, hapa kila mtu ni muhimu sana! Mtume Paulo anawafundisha waamini tunu msingi za Kiinjili zinazopaswa kuzingatiwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko kati kati yao na kadiri walivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zake walio wadogo, wamemtendea Kristo Mwenyewe! Huu ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini kama ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa maskini ambao pia ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo. Ni mwaliko wa kutambua na kuonja maumivu ya jirani zao; kufurahi na kutukuzwa kwa ndugu zao. Pasiwepo na mashindano yasiokuwa na tija wala mashiko, bali kwa unyenyekevu, kila mtu amheshimu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Waamini wawe na nia moja ndani yao ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu.

Imani inarutubishwa kwa njia ya matumaini kwa kutambua kwamba, kilio cha maskini ni kilio cha matumaini yanayofumbatwa katika upendo wa Mungu anaojiaminisha kwake. Mtakatifu Theresa wa Avila anasema, umaskini ni amana inayofumbata mema ya duniani na kumhakikishia mwamini uwezo wa kuratibu mali za dunia bila kuonesha dharau. Waamini wawe na mang’amua ya kutambua mema kwa ajili ya wao wenyewe, wengine na wale wanaowazunguka.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wakleri na hasa mashemasi kwamba, wamewekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa maskini kwa kushirikiana na watawa pamoja na vyama na mashirika mbali mbali ya kitume ili kujibu kilio cha maskini kama njia muafaka ya utekelezaji wa mchakato wa uinjilishaji mpya. Maskini wanaliinjilisha Kanisa na kuwasaidia waamini kugundua kila siku uzuri wa Injili na kwamba, hii ni siku mahususi kwa waamini kujipatia neema, kwa kuwaonyooshea maskini mkono wa ukarimu, ili kuenzi imani na kumwilisha upendo, ili kukoleza matumaini, ili kusonga mbele na hija ya kukutana na Kristo Yesu anayekuja!

Maskini Duniani 2018
15 November 2018, 07:28