Tafuta

Papa Francisko: Siku ya II ya Maskini Duniani 2018: Kilio, Kujibu na Kuokoa! Papa Francisko: Siku ya II ya Maskini Duniani 2018: Kilio, Kujibu na Kuokoa! 

Maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani 2018: Sikilizeni na kujibu kilio cha maskini!

Baba Mtakatifu Francisko, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Pili ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita na Bwana akamsikia”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Upendo ni sumaku inayomuunganisha Mungu na binadamu, changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, ameamua kuanzisha Siku ya Maskini Duniani, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya XXXIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kabla ya maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayofunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa.

Siku hii kwa Mwaka 2018 inaadhimishwa Jumapili, tarehe 18 Novemba 2018. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni: “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia”. Zab. 34: 6 (Katika Biblia ya Kiswahili). Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Pili ya Maskini Duniani kwa mwaka 2018, anakazia mambo makuu matatu: Kilio, Kujibu na Kuokoa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kuungana pamoja na Mwenyezi Mungu,  ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Mungu ili kusikiliza kilio cha maskini kwa kuwaokoa na kuwajengea uwezo wa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya kijamii. Hata leo hii kuna maskini wanaojitambulisha kama akina: Bartimayo kipofu, aliyepaaza sauti yake, kiasi hata cha kumfikia Yesu, akamponya upofu wake, akapata kuona tena. Hata leo hii pia kuna watu ambao hawana: fursa za ajira wala fedha ya kutosheleza mahitaji yao msingi na matokeo yake, wengi wao wanatumbukizwa kwenye utumwa mamboleo! Wote hawa bado wanayo matumaini ya mtu anayeweza kuwaambia !Jipe moyo; inuka, anakuita!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya anasema, Siku ya Maskini Duniani ni mwaliko kwa Kanisa na waamini katika ujumla wao, kujibu kilio cha maskini kwa vitendo! Ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu Francisko anafafanua aina mbali mbali za umaskini na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu. Kwa bahati mbaya, mali na utajiri wa ulimwengu huu, unawapofusha watu wengi, kiasi cha kujifungia katika ubinafsi wao. Kilio cha maskini kijenge utamaduni wa kusikiliza na kujibu kwa njia ya kukutana na watu.

Kwa kawaida maskini ni watu wa kwanza kuonja na kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao, kiasi hata cha kuweza kutolea ushuhuda wa maisha yao, hata nyakati za giza na usiku mnene, daima atawakirimia upendo na faraja yake. Lakini, ili kuweza kupata ukombozi wa kweli, kuna haja ya kuwepo na watu ambao  wataweza kujisadaka kuwasikiliza, kwa kuwafungulia malango ya nyoyo na maisha yao, ili kuwawezesha kujisikia kuwa ni marafiki, ndugu na jamaa. Kwa njia hii watawaweza kuonja nguvu inayokoa na kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa.

Huu ni ujumbe wa matumaini unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko anasema, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella. Maskini wanaomlilia na kumtafuta Mungu katika maisha yao, atawajibu kwa wakati muafaka; atawaokoa na kuwajalia maisha tele! Siku ya Maskini Duniani inaadhimishwa kwa kutana na jirani. Jumapili tarehe 18 Novemba 2018 atakutana na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na vyama na mashirika ya kitume yanayojihusisha kwa namna ya pekee na huduma kwa maskini. Baba Mtakatifu atashiriki chakula cha mchana na maskini 3, 000.

Jumamosi, tarehe 17 Novemba 2018 kutakuwa na mkesha wa sala kwenye Kanisa kuu la “Mtakatifu Lorenzo Fuori le mura”. Kwa muda wa Juma zima yaani kuanzia tarehe 12- 18 Novemba 2018 katika Uwanja wa Pio wa XII, kutawekwa hema kwa ajili ya huduma ya afya. Mwaka 2017 wagonjwa 600 waliweza kupima afya zao na kupatiwa tiba. Huduma hii itatolewa bure na Madktari kutoka Vatican, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Gemeli pamoja na Chuo Kikuu cha Tor Vergata.

Kardinali Basetti anakaza kusema, Siku ya Maskini Duniani inapaswa kuwa ni siku ya kutafakari jinsi ya kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, kwa kujenga na kudumisha matendo ya huruma: kiroho na  kimwili. Huu utakuwa ni mwendelezo sahihi wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha neema na baraka. Ni wakati wa kufungua akili na nyoyo za watu ili kuangalia ni kwa jinsi gani huruma ya Mungu, inaweza kumwilishwa katika matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji na ushuhda wenye mvuto na mashiko wa uinjilishaji mpya. Upendo unaongoza, sheria inatekeleza!

Siku ya Maskini Duniani 2018
12 November 2018, 09:14