Tafuta

Papa Francisko: Siku ya Maskini Duniani 2018: Kusikia na kujibu kilio cha maskini ni hitaji la kitaalimungu! Papa Francisko: Siku ya Maskini Duniani 2018: Kusikia na kujibu kilio cha maskini ni hitaji la kitaalimungu! 

Siku ya Maskini Duniani: Kusikiliza na kujibu kilio cha maskini ni hitaji la kitaalimungu!

Hiki ni kilio cha wazee wanaoteseka kwa upweke hasi; ni kilio cha watu wanaopambana na changamoto za maisha pasi na marafiki. Hiki ni kilio cha wakimbizi na wahamiaji; kilio cha watu wanaopokwa utajiri na rasilimali ambazo zingesaidia kupambana umaskini. Hiki ni kilio cha akina Lazaro maskini, wakati matajiri wakiponda mali, eti kufa kwaja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani kwa mwaka 2018 inayoongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia” sanjari na kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 18 Novemba 2018 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa “maskini” amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu yaliyofanywa na Yesu kama ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini: Mosi, aliacha yote na kujitenga kwa ajili ya sala; Pili, Yesu aliwaendea Mitume wake waliokuwa wanatembea katika giza la usiku wa manane na; Tatu, Yesu aliwaokoa, hasa pale Petro alipokua anazama majini kutokana na imani haba, changamoto na mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Mosi, aliacha yote na kujitenga kwa ajili ya sala: Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kristo Yesu, baada ya kufanya ule muujiza wa kugeuza mikate mitano na samaki wawili na kuwalisha watu zaidi elfu tano, akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni! Yesu akapanda mlimani faraghani, ili kusali, lakini kati kati ya usiku wa manane, akawaendea wanafunzi wake waliokuwa wanataabika kutokana na upepo wa mbisho, akaukemea na hatimaye, akawatuliza wanafunzi wake.

Yesu anawafundisha wanafunzi wake kuondokana na mafanikio mpito yanayoweza “kuwavimbisha kichwa na kuufanya moyo wa upendo na huduma kulala katika usingizi”. Yesu alikwenda kusali kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwaombea maskini, huku akiwaacha wanafunzi wake waendelee na safari ya kwenda kwa Baba huku wakiwa wepesi kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo kwamba, tangu sasa wao si wageni wala wapitaji, bali ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu! Baba Mtakatifu analichangamotisha Kanisa kujitosa na kuachilia yote na hatimaye, kuanza kujikita katika huduma kwa Mungu na jirani.

Pili, Yesu aliwaendea Mitume wake waliokuwa wanatembea katika giza la usiku wa manane, huku wakipambana na nguvu za giza! Kwa maneno mengine, Yesu aliwaendea wanafunzi wake, huku akivunjilia mbali nguvu za giza. Huu ni ufunuo na uhakika kwamba, Kristo Yesu anazo nguvu na uweza wa kuvunjilia mbali nguvu za shetani, dhambi, kifo na woga! Hata leo hii, Yesu anapenda kuwaambia wafuasi wake: “Jipeni moyo, ni mimi msiogope”! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, maisha ya mwanadamu daima yanakumbwa na mawimbi mazito, kuna wakati yanapata utulivu na baadaye, mawimbi yanaendelea kuwazonga watu, kiasi cha kuwatia hofu na mashaka.

Siri ya amani na utulivu wa ndani wakati wa safari kwenye mawimbi mazito ya bahari ya maisha, ni kumwalika Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia waja wake, zawadi ya maisha dhidi ya kifo na matumaini wakati wa shida na mahangaiko. Yesu peke yake ndiye anayeweza kuganga na kuponya moyo uliovunjika na kupondeka kwa njia ya msamaha; anamweka mtu huru kwa njia ya imani thabiti. Waamini wakiwa na Yesu chomboni, mambo yote ni shwari na hivyo kuwa hata na uwezo wa kuwaendea jirani kwa ajili ya kuwasaidia. Walimwengu wanahitaji watu wanaoweza kuwafariji si tu kwa maneno matupu, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Kwa jina la Yesu, watu wanaweza kutoa faraja ya kweli kwa wale wanaoteseka!

Tatu, Yesu aliwaokoa, hasa pale Mtakatifu Petro alipokua anazama majini kutokana na imani haba, kielelezo cha waamini wenye imani haba na maskini wanaonyoosha mikono yao ili kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwakomboa katika shida na mahangaiko yao, chemchemi ya imani anasema Baba Mtakatifu. Huu ni mwanzo wa wongofu wa ndani kwa kujiondoa kabisa kutoka katika kiburi, hali ya kujiamini kupita kiasi na kujiona kuwa si mali kitu! Mtu anayehitaji wokovu na mkono wenye nguvu utakaomwokoa kutoka katika “majanga ya maisha”. Hali hii inawezekana pale tu mtu anapojitambua kwamba, ni mhitaji na hivyo kuthubutu kuomba msaada!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwilisha imani yao katika matendo, kwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hili si hitaji la kijamii wala la Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa nyakazi hizi, bali ni hitaji la kitaalimungu. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni waombaji wa wokovu na ndugu ya wote, lakini zaidi maskini ambao wana upendeleo wa pekee, machoni pa Mwenyezi Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, roho ya ufukara na mapendo ndio utukufu na ushuhuda wa Kanisa la Kristo!

Yesu alisikiliza na kujibu kilio cha Mtakatifu Petro aliyekuwa anazama katika tumbo la bahari, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusikiliza na kujibu hasa kilio cha watoto ambao wanatupwa mimba kutokana na utamaduni wa kifo; kilio cha watu wanaoteseka kwa baa la njaa na utapiamlo duniani; watoto wanaokufa kwa kupewa mabomu kuchezea badala ya michezo ya watoto. Hiki  ni kilio cha wazee wanaoteseka kwa upweke hasi; ni kilio cha watu wanaopambana na changamoto za maisha pasi na marafiki. Hiki ni kilio cha wakimbizi na wahamiaji; kilio cha watu wanaopokwa utajiri na rasilimali ambazo zingesaidia kupambana umaskini. Hiki ni kilio cha akina Lazaro maskini, wakati matajiri wakiponda mali, eti kufa kwaja!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukosefu wa haki msingi za binadamu ni chanzo cha umaskini wa kutupwa. Kilio cha maskini kinaendelea kuongezeka kila kukicha, lakini kwa bahati mbaya, watu wanaokisikiliza wanaendelea kupungua siku hadi siku; maskini wanaongezeka, lakini utajiri wa ulimwengu unaendelea kukumbatiwa na watu wachache sana duniani! Mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani, mwamini anapaswa kunyoosha mkono wake, kusikiliza na kujibu kilio hiki kwa matendo.

Yesu anawataka wafuasi wake wamtambue kati ya maskini; watu wenye njaa na kiu ya haki; wageni na wale wote ambao wanapokwa utu na heshima yao kama binadamu; wagonjwa na wafungwa! Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Yesu anawataka wafuasi wake kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma na upendo kwa maskini na hii ndiyo hazina wanayoweza kujiwekea mbinguni.

Papa: Misa Makini
18 November 2018, 13:17