Tafuta

Siku ya Maskini Duniani 2018: Chakula cha mchana, alama ya umoja, upendo na mshikamano wa kidugu! Siku ya Maskini Duniani 2018: Chakula cha mchana, alama ya umoja, upendo na mshikamano wa kidugu! 

Siku ya Maskini Duniani 2018: Mshikamano wa umoja, udugu na upendo wa kidugu!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 18 Novemba 2018, ameshiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa ajili ya maskini, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo, kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kupata nafasi ya kukaa pamoja kwa amani na utulivu, ili kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, ukosefu wa haki msingi za binadamu ni chanzo cha umaskini wa kutupwa. Kilio cha maskini kinaendelea kuongezeka kila kukicha, lakini kwa bahati mbaya, watu wanaokisikiliza wanaendelea kupungua siku hadi siku; maskini wanaongezeka, lakini utajiri wa ulimwengu unaendelea kukumbatiwa na watu wachache sana duniani! Mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani, mwamini anapaswa kunyoosha mkono wake, kusikiliza na kujibu kilio hiki kwa vitendo!

Baba Mtakatifu baada ya kuadhimisha Misa Takatifu na maskini kutoka ndani na nje ya Roma, waliokuwa wamesindikizwa na vyama, mashirika na vikundi vya kujitolea, wakati wa mchana ameshiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa ajili ya maskini, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo, kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kupata nafasi ya kukaa pamoja kwa amani na utulivu, ili kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake. Tukio hili limefanyika pia kwenye Parokia na vituo vya huduma kwa maskini sehemu mbali mbali za dunia, kama njia ya kuenzi Siku ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2018 iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2016 kama matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Ukumbi wa Paulo VI, amemshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na watu mbali mbali waliojisadaka ili kufanikisha tukio hili la kihistoria katika maadhimisho ya Siku ya II ya Maskini Duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, watu 1,500 wameshiriki chakula hiki, kwa kuhudumiwa na vijana wa kujitolea 70 kutoka katika Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, mashirika pamoja na vyama vya kujitolea. Muziki umeporomoshwa na Bendi ya Muziki kutoka katika Madhabahu ya Pompei. Mwishoni mwa chakula, Baba Mtakatifu amewazawadia waliohudhuria mifuko ya chakula, amewasalimia watoto na maskini na baadaye akawapa baraka yake ya kitume, na kuondoka kwenda kujipumzisha!

Papa: Chakula maskini

 

 

19 November 2018, 12:07