Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Heri za Mlimani ni dira na mwongozo katika hija ya utakatifu wa maisha! Papa Francisko asema, Heri za Mlimani ni dira na mwongozo katika hija ya utakatifu wa maisha!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Siku kuu ya watakatifu wote ni sherehe ya familia!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata “Heri za Mlimani”: Muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, chemchemi ya umaskini wa roho, rehema na moyo safi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Novemba anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Wote, wito na mwaliko kwa watu wote kuwa ni watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kumwilisha Matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yao sanjari na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawataka waamini kujitoa kwa moyo wote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma ya jirani!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe Alhamisi, tarehe Mosi Novemba, 2018 amesema, Liturujia ya Neno la Mungu katika maadhimisho ya Siku kuu hii inawaonesha watakatifu kuwa ni umati mkubwa sana wa watu wa kila taifa, kabila, jamaa na lugha, ambao walikuwa wanamsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu, dhamana inayotekelezwa na waamini wanaposhiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Waamini wanaungana na watakatifu wote walioandikwa kwenye Kalenda ya Liturujia ya Kanisa na wale ambao bado hawajaandikwa na hawa ni jirani, ndugu na jamaa zao, ambao wanaunda umati mkubwa wa watu wanaomtukuza na kumsifu Mungu. Kutokana na mantiki hii, Siku kuu ya Watakatifu Wote anasema Baba Mtakatifu Francisko ni Siku kuu ya Familia. Watakatifu ni watu ambao wako karibu nao na ndugu zao wa kweli; wanaowafahamu na kuwapenda; wanaotambua mahitaji yao msingi; wanaowasaidia na kuwasubiri kwa mikono miwili; huku wakiwa na furaha ya kutaka kukutana nao huko Paradiso!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata “Heri za Mlimani”: Muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, chemchemi ya umaskini wa roho, rehema na moyo safi. Lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, Heri za Mlimani zinasigana sana na matamanio ya walimwengu yanayojikita zaidi katika utajiri, nguvu na madaraka, udanganyifu; watu wanaopenda kuogelea katika raha na starehe za ulimwengu huu. Njia ya Heri za Mlimani na Hija ya Utakatifu wa maisha, zinaonekana kana kwamba, hazina nguvu tena! Lakini, Neno la Mungu linakaza kusema, watakatifu wamevikwa mavazi meupe na wana matawi ya mitende mikononi mwao, alama ya ushindi dhidi ya ulimwengu, kwani wameamua kumchagua Mungu ambaye ni Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiuliza wao, wako upande gani? Na ikiwa kama kweli wanataka kuambata na kuchuchumilia utakatifu, au wanaridhika kuwa Wakristo, wanaomwamini Mungu na kuwapenda jirani zao kwa maneno tu?

Kristo Yesu anataka makubwa kutoka kwa wafuasi wake, kwani Yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli! Baba Mtakatifu anawataka waamini kukumbatia utakatifu wa maisha kwa kuchagua kuwa upande wa Mungu: huku wakiendelea kujivika fadhila ya unyenyekevu, upole, huruma na usafi kamili, kwani wanavutwa zaidi na maisha matakatifu kuliko kukubali kumezwa na malimwengu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watakatifu wanawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha Injili katika matendo, huku wakiongozwa na “Heri za Mlimani” zinazomwilishwa katika uhalisia wa  maisha ya kila siku katika familia na nyumbani. Binadamu ameumbwa si kwa ajili ya kifo, bali kufurahia maisha ya uzima wa milele. Jamani, furahini na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa watakatifu, awasaidie waamini kuambata na kukumbatia njia ya utakatifu wa maisha, kwani yeye ni mlango wa mbingu, asaidie kuwapokea na kuwakaribisha marehemu katika familia ya mbinguni!

Siku kuu ya watakatifu
01 November 2018, 17:26