Tafuta

Papa Francisko: Hata wale wanaonyimwa uhuru wa kuabudu na kidini ni mashuhuda wa imani! Papa Francisko: Hata wale wanaonyimwa uhuru wa kuabudu na kidini ni mashuhuda wa imani! 

Papa Francisko hata wale wanaonyimwa uhuru wa kuabudu ni mashuhuda wa imani!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, idadi ya Wakristo wanaouwawa kila siku inaongezeka maradufu. Mashuhuda wa imani ni wale ambao pia wananyimwa uhuru wa kidini na kuabudu hata katika nchi zile ambazo zinajidai kwamba, zina demokrasia ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalem “Order of the Holy Sepulchre of Jerusalem” limekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma ya upendo na maisha ya kiroho kwa familia ya Mungu inayoishi katika Nchi Takatifu. Washauri wakuu wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalemu wanaofanya mkutano wao mkuu kila baada ya miaka mitano, Ijumaa, tarehe 16 Novemba 2018 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amewapongeza kwa kazi kubwa wanazozitenda na kwamba, idadi ya wanachama wao imeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2013.

Idadi hii imekwenda sanjari na upanuzi wa shughuli na utume wa Shirika hasa kwenye maeneo ambayo yako pembezoni mwa jamii huko katika Nchi Takatifu pamoja na kuendeleza utamaduni wa kufanya hija kama sehemu ya maboresho ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa mchango wao wa huduma katika shughuli za kichungaji na kitamaduni na anawataka kuendelea na moyo huu, pamoja na kumsaidia Patriaki wa Yerusalemu kuweza kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, ambalo katika kipindi cha miaka mitano limelilazimisha Kanisa kutoa majibu muafaka ya huduma kwa watu hawa huko Mashariki ya Kati!

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kuendelea kujisadaka katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo pasi na ubaguzi wa kidini, kielelezo makini cha ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazomwilishwa katika huduma; majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika mkutano wao, wamejikita zaidi katika dhamana na nafasi ya wafanyakazi mahalia, wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi zaidi ya 30, ushuhuda wa upyaisho wa huduma inayotolewa na Shirika.

Baba Mtakatifu amewataka kukuza na kudumisha maisha ya kiroho ya wanachama wake, ili kudumisha uhusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na uelewa makini wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Viongozi wakuu wa Shirika wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa maneno na matendo yao, ili kuonesha kwamba, kweli uongozi ni huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu!

Huduma ya upendo inayotolewa na Shirika hili haina budi kujikita katika Injili ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda wa wema na upendo wa Mungu anayewapenda wote pasi na ubaguzi. Shirika hili ambalo linawashirikisha hata wakleri ni kielelezo cha huduma ya kichungaji inayowawajibisha kujenga maisha ya sala za kijumuiya, liturujua inayoadhimishwa katika ngazi mbali mbali, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kukombolewa; mazoezi ya maisha ya kiroho na katekesi endelevu ni muhimu sana katika majiundo ya maisha na ukuaji wa wanachama wao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, idadi ya Wakristo wanaouwawa kila siku inaongezeka maradufu. Mashuhuda wa imani ni wale ambao pia wananyimwa uhuru wa kidini na kuabudu hata katika nchi zile ambazo zinajidai kwamba, zina demokrasia ya kweli. Baba Mtakatifu anasema, yuko pamoja nao kwa njia ya sala na wasichoke kumwomba Bikira Maria wa Palestina, msaada wa Wakristo, ili awaombee nguvu na faraja wakati wa mateso na mahangaiko yao. Bikira Maria aendelee kuwaombea wale wote ambao uhuru wa kidini uko mashakani na daima wanatembea katika hofu ya kifo.

Papa: Kaburi Takatifu
16 November 2018, 15:28