Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika upendo, haki na amani. Papa Francisko: Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika upendo, haki na amani. 

Papa Francisko: Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika upendo, haki na amani

Mungu ni upendo na anataka kuanzisha na kujenga ufalme wa: upendo, haki na amani utakaodumu hadi mwisho wa nyakati! Baba Mtakatifu anasema, historia inaonesha kwamba, falme ambazo zimejengwa kwa nguvu ya “mtutu wa bunduki”, zimedumu kwa kitambo na mwishowe, zitaporomoka na kutoweka katika uso wa dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwishoni mwa Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, waamini wanaadhimisha Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu wote! Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kana kwamba, alikua anawania madaraka ya kisiasa, yaani, kuwa ni mfalme wa Wayahudi! Ni kutokana na wasi wasi huu, Pilato alimuuliza Yesu mara mbili, ikiwa kama kweli Yeye ni mfalme!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Kristo Mfalme, tarehe 25 Novemba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, Yesu alimjibu akamwambia kwamba, ufalme wake si wa ulimwengu huu na kuwa yeye amesema kwamba, ni mfalme. Huu ni ukweli ulioambata maisha ya Yesu tangu mwanzo! Alipofanya muujiza na kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, watu walitaka kumkamata ili wamtangaze kuwa mfalme, lakini Yesu akajitenga na umati na kwenda kusali faraghani.

Ufalme wa Yesu haufumbatwi katika vurugu, fujo na vita na ndiyo maana wafuasi wake, hawakupigana vita ili kumlinda! Yesu anakaza kusema, ikiwa kama ufalme wake ungekuwa ni wa ulimwengu huu, watumishi wake wangelimpigania, ili asitiwe mikononi mwa Wayahudi. Hapa Yesu alitaka kuonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni mkuu na ana nguvu zaidi kuliko viongozi wa kisiasa na kwamba, ufalme wake haujengwi kwa nguvu za kibinadamu! Kristo Yesu amezaliwa kwa ajili ya hayo, ili kuonesha nguvu ya upendo wa Mungu na kushuhudia kweli.

Huu ndio ukweli wa Kimungu na kiini cha Injili, kwamba, Mungu ni upendo na anataka kuanzisha na kujenga ufalme wa: upendo, haki na amani utakaodumu hadi mwisho wa nyakati! Baba Mtakatifu anasema, historia inaonesha kwamba, falme ambazo zimejengwa kwa nguvu ya “mtutu wa bunduki”, zimedumu kwa kitambo na mwishowe, zitaporomoka na kutoweka katika uso wa dunia! Ufalme wa Mungu unafumbatwa katika upendo na kujikita katika sakafu ya nyoyo za watu na hivyo kuwakirimia wote wanaoupokea amani, uhuru wa kweli na utimilifu wa maisha. Binadamu wataweza kupata: amani, uhuru na utimilifu wa maisha ikiwa kama watatoa nafasi kwa upendo na ufalme wa Mungu uweze kukita mizizi katika nyoyo zao; ikiwa kama ufalme wa Kristo utazamisha mizizi yake katika nyoyo za watu, watafanikiwa kupata amani, uhuru na utimilifu wa maisha!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwachia nafasi Yesu Kristo Mfalme, ili aweze kutawala katika nyoyo zao! Huyu ndiye ambaye kwa njia ya maisha, maneno na matendo yake ametundikwa Msalabani, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Fumbo la Msalaba linaonesha dira na mwongozo wa maisha kwa watu waliopoteza dira na kutembea katika hofu na mashaka yanayowaandama kila kukicha. Ufalme wa Kristo Yesu si wa ulimwengu huu, kwani ana uwezo wa kutoa mwelekeo mpya wa maisha, hata katika majaribu na mashaka, jambo la msingi ni kufuata mwongozo wa ufalme wake.

Papa: Kristo Mfalme

 

25 November 2018, 08:38