Vatican News
Papa Francisko: Maisha yenu yawe ni sadaka inayofumbata unyenyekevu na ukarimu! Papa Francisko: Maisha yenu yawe ni sadaka inayofumbata unyenyekevu na ukarimu!  (ANSA)

Papa Francisko: Sadaka ya maisha yenu iwe ni kielelezo cha unyenyekevu na ukarimu!

Yesu anapenda kukazia mambo msingi katika maisha yanayojenga na kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu anayeangalia ubora na wala si wingi; anayechunguza dhamiri na kuridhika na nia njema. Hii ndiyo maana halisi ya kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka na huduma kwa jirani bila kutaka kujikweza,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili XXXII ya Mwaka B wa Kanisa inafunga muhtasari wa Mafundisho makuu yaliyotolewa na Kristo Yesu kwenye Hekalu la Yerusalemu na kwa namna ya pekee, anayaangalia makundi mawili ya watu: Waandishi na Mjane. Waandishi wana wakilisha watu maarufu, matajiri na wenye nafasi katika jamii, hao hupenda kuketi mbele ya masinagogi na viti vya mbele katika karamu na kwa unafiki husali sala ndefu. Hili ni kundi la watu linalotaka kumtumia Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao binafsi, ili kupewa heshima kwa kujikweza na kuwadharau wengine kuwa si mali kitu! Lakini mjane anasimama badala ya maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali na nafasi katika jamii.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 11 Novemba 2018. Kristo Yesu katika mafundisho yake, anawaumbua waandishi kwani walitumia nafasi zao kwa ajili ya kuwanyonya na kuwakandamiza maskini kwa kutumia mgongo wa dini. Yesu anatumia mfano wa mjane, ambaye hakuwa na mtu wa kutetea haki zake msingi, ndiye mwanamke aliyeonesha ujasiri wa kutoa sadaka safi iliyompendeza hata Yesu mwenyewe.

Ni katika unyenyekevu huu, mjane anatoa sadaka ambayo inabeba umuhimu wa pekee katika maisha ya kidini na kiroho, kiasi hata cha kung’ara mbele ya Yesu na kuwa ni mfano bora wa kuigwa! Yesu anapenda kukazia mambo msingi katika maisha yanayojenga na kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu anayeangalia ubora na wala si wingi; anayechunguza dhamiri na kuridhika na nia njema. Hii ndiyo maana halisi ya kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka na huduma kwa jirani bila kutaka kujikweza, bali kielelezo cha sadaka na majitoleo binafsi, kama ambavyo Kristo Yesu amefanya kwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Kristo Yesu kwa njia ya Damu yake Azizi amewakomboa bure wanadamu wote, kumbe, wafuasi wake, wanapaswa kutenda vyema kama kielelezo cha shukrani. Mjane anakuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mjane huyu, hakutajwa jina, bila shaka yuko mbinguni, changamoto na mwaliko kwa waamini kuvijika utu wema na unyenyekevu wa moyo, kwa kuondokana na mambo yasiyokuwa na uzito, ili hatimaye, kuambata mambo msingi katika maisha, yaani kuwa wanyenyekevu! Bikira Maria, mwanamke maskini, aliyethubutu kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi, awasaidie waamini kumtolea Mwenyezi Mungu na jirani zao, sehemu muhimu ya maisha yao katika unyenyekevu na ukarimu!

Papa: Mjane
12 November 2018, 08:37