Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, tarehe 15 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Reuven Rivlin wa Israeli. Papa Francisko, tarehe 15 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Reuven Rivlin wa Israeli.  (ANSA)

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais wa Israeli mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais Rivlin, yalijikita zaidi katika maandalizi ya Jubilei ya miaka 25 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Israeli na kwamba, hadi sasa wameridhika na hali hii lakini maboresho makubwa yanaweza kufanywa zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Reuven Rivlin wa Israeli, ambaye baadaye alipata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais Rivlin, yalijikita zaidi katika maandalizi ya Jubilei ya miaka 25 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Israeli na kwamba, hadi sasa wameridhika na hali hii!

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamesema, kuna haja ya kuboresha uhusiano kati ya Serikali na jumuiya za kikristo nchini Israeli na kwamba, hivi karibuni, wataweza kuafikiana kuhusu mambo msingi yanayogusa mafao ya pande hizi mbili. Kumbe, ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa pande hizi mbili kuaminiana na kwamba, majadiliano kati ya Israeli na Palestina yanapaswa kufikia muafaka, kwa kuheshimu mawazo ya wananchi wa pande hizi mbili. Viongozi hawa wamegusia mji wa Yerusalemu na umuhimu wake katika maisha ya kiroho na kiutu kati ya Wayahudi, Wakristo na Waislam na kwamba, kuna umuhimu kwa Yerusalemu kudumisha hadhi yake kama Mji wa Amani.

Mwishoni mwa mazungumzo ya viongozi hawa wawili, yalijielekeza zaidi katika masuala ya kisiasa na kijamii katika Ukanda wa Mashariki ya Kati, ambao umegubikwa kwa vita pamoja na kinzani mbali mbali na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Katika mazingira kama haya viongozi hawa wamekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya waamini wa dini mbali mbali huko Mashariki ya Kati, ili amani na utulivu viweze kurejea tena!

Papa: Rais Israeli

 

16 November 2018, 14:23