Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Umoja wa Wakristo ni utashi wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake! Papa Francisko: Umoja wa Wakristo ni utashi wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake! 

Siku kuu ya Mt. Andrea: Umoja wa Wakristo ni utashi wa Yesu kwa wafuasi wake!

Huu ni umoja unaopaswa kujionesha katika mshikamano na watu wanaoteseka kwa umaskini, magonjwa, njaa na vita. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Kusali na Kufunga kwa Ajili ya Mashariki ya Kati, iliyofanyika tarehe 7 Julai 2018 huko Bari, Kusini mwa Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Vatican ukiongozwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, tarehe 30 Novemba 2018, umeshiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Andrea Mtume, inayopewa uzito wa pekee na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kama msimamizi wa Kanisa hilo. Liturujia Takatifu imeongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na ujumbe wa Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya ukasomwa na  Kardinali Kurt Koch ambamo Baba Mtakatifu Francisko anaonesha furaha kwa Mtakatifu Andrea aliyeitwa wa kwanza na kumshikirisha wito huu ndugu yake Petro, wote wawili wakajisadaka kwa ajili ya kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anasema, ushiriki wa Vatican katika maadhimisho haya ni sehemu ya utamaduni wa Makanisa haya mawili, kama kielelezo cha umoja na chachu ya kusonga mbele katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuvunjilia mbali uhasama, kinzani na ukimya uliotawala kati ya Makanisa haya mawili kwa miongo kadhaa iliyopita. Roho Mtakatifu chemchemi ya umoja, ndiye aliyewawezesha kuanza tena mchakato wa majadiliano ya kidugu, kielelezo cha ujasiri wa imani uliooneshwa na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Patriaki Athenagoras, walioyawezesha Makanisa haya mawili kugundua tena kifungo cha umoja uliokuwepo tangu awali kati ya Wakristo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Makanisa yamedumisha Mapokeo kwa uangalifu mkubwa pamoja na kutunza Mafundisho ya Mitaguso Mikuu ya Kwanza sanjari na Nyaraka za Mababa wa Kanisa, ingawa kumekuwepo na mwendelezo tofauti wa Mafundisho ya Mababa wa Kanisa mintarafu Makanisa mahalia na kwamba, Mafundisho haya hayana budi kufafanuliwa kwa kina na mapana! Wakristo wote watambue kwamba, wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kushikamana ili kutafuta na kudumisha misingi ya amani; kwa kubomolea mbali mifumo ya utumwa mamboleo, ili utu, heshima na haki msingi za binadamu ziweze kukuzwa na kudumishwa pamoja na kutunza mazingira nyumba ya wote!

Kwa neema ya Mungu na kwa njia ya kukutana na kujadiliana, dhamana ambayo imetekelezwa na Makanisa haya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, waamini wameanza kuonja umoja ambao unapaswa kukamilishwa sasa! Ikumbukwe kwamba, huu ni utashi wa Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja. Huu ni umoja unaopaswa kujionesha katika mshikamano na watu wanaoteseka kwa umaskini, magonjwa, njaa na vita. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Kusali na Kufunga kwa Ajili ya Mashariki ya Kati, iliyofanyika tarehe 7 Julai 2018 huko Bari, Kusini mwa Italia na kuhudhuriwa na Wakuu wa Makanisa ya Mashariki ambako bado watu wanateseka sana! Katika ulimwengu ambao umejeruhiwa sana na vita pamoja na kinzani mbali mbali, umoja wa Wakristo ni alama ya matumaini ambayo yanapaswa kung’ara zaidi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kumhakikishia Patriaki Bartolomeo wa kwanza uwepo wake kwa njia ya sala, ili Mwenyezi Mungu ambaye ni kisima cha upatanisho na amani, awakirimie nia moja, ili wawe ni watu wanaohurumiana na kupendana kama ndugu; wasikivu na wanyenyekevu kwa sababu haya ndiyo urithi na baraka!

Papa: Mtakatifu Andrea

 

30 November 2018, 16:19