Vatican News
Papa Francisko: Maskini wapewe kipaumbele kwani wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa! Papa Francisko: Maskini wapewe kipaumbele kwani wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa!  (ANSA)

Papa Francisko: Maskini wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa!

Kanisa linapaswa kuwa maskini na kwa ajili ya maskini, ili: kuwapokea, kuwasikiliza, kuwatetea na hata kuthubutu kuinjilishwa nao, kwa kutambua nguvu ya kuokoa inayofumbatwa katika maisha yao sanjari na hekima ya Mungu anayotaka kuwashirikisha watu wake kwa njia ya maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkondo wa Utume kwa Vipofu, MAC. unaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 90 tangu kuanzishwa kwake na Maria Motta, mwanamke aliyekuwa na ulemavu wa macho, lakini jasiri katika maisha na matendo yake, kiasi cha kujikita katika mafundisho ya Kanisa na kuanzisha mkondo huu, kunako mwaka 1928 na kuidhinisha na Mtakatifu Yohane XXIII, kwa lengo la walemavu wa macho nchini Italia kuweza kufarijiana na kusaidiana katika safari yao ya maisha. Alitaka walemavu hawa kujitegemea ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani hata katika ulemavu wao.

Leo hii mkondo wa Utume kwa Vipofu unawajumuisha wale wanaoona na walemavu, ili kushirikishana pamoja na kuwaendeleza watu wenye ulemavu wa macho, ili kujenga na kudumisha urafiki wa kikristo unaofumbatwa katika hija ya majiundo ya imani katika maisha yao! Silaha kubwa inayowaunganisha ni upendo wa kweli, unaomwilishwa katikaa uhalisia wa maisha sanjari na kuheshimiana. Kila mtu anapokelewa na kuthaminiwa jinsi alivyo, kiasi hata cha kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa jamii kadiri ya hali na mazingira yake, ili kuwawapatia watu wenye ulemavu wa macho matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, daima wakijitahidi kuwa na furaha katika maisha yao!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 17 Novemba 2018 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkondo wa Utume kwa Vipofu, ambao kweli ni wafuasi na mitume wa Injili, watu ambao ni wakarimu hata kwa maskini zaidi yao kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Badala ya kujiangalia wao wenyewe, wameonesha ujasiri wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yao kama chachu ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Imegota miaka 50 ya ushirikiano na maskini kutoka katika nchi changa zaidi duniani.

Katika kipindi cha miaka 90 ya uwepo na utume wake, MAC imeweza kujikita katika kukuza na kudumisha umoja na mshikamano pamoja na ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, kiasi cha kuliwezesha Kanisa kati pamoja na maskini kuendelea kukua na kuongekeza na kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji unaojikita katika mapendo ya Kikristo na kama unavyodokezwa katika Fumbo la Umwilisho. Kanisa linapaswa kuwa maskini na kwa ajili ya maskini, ili: kuwapokea, kuwasikiliza, kuwatetea na hata kuthubutu kuinjilishwa nao, kwa kutambua nguvu ya kuokoa inayofumbatwa katika maisha yao sanjari na hekima ya Mungu anayotaka kuwashirikisha watu wake kwa njia ya maskini!

Mkondo wa Utume kwa Vipofu, MAC umeendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya huduma kwa maskini ndani na nje ya Italia; kwa kushirikiana na walemavu kutoka katika majimbo mbali mbali nchini Italia pamoja na kushikamana na wamisionari katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, dhamana na utume ambao umeendelezwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kama njia ya kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika uhalisia wa maisha. Mwelekeo huu umetoa kipaumbele cha pekee kwa maskini duniani, hasa wale wenye ulemavu wa macho!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yote haya yanasaidia kujenga sanaa na utamaduni wa ukarimu unaofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, changamoto na mwaliko kwa watu wote kuwasaidia na kuwahudumia maskini! Ikumbukwe kwamba, ustawi na maendeleo ya watu kwa siku za mbeleni yanafumbatwa katika mshikamano na urafiki, lakini zaidi na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Papa: Utume kwa Vipofu
17 November 2018, 15:41