Papa Francisko: Jiandaeni kumpokea Bwana arusi mkiwa na mafuta ya akiba! Papa Francisko: Jiandaeni kumpokea Bwana arusi mkiwa na mafuta ya akiba! 

Papa Francisko: Wekeni akiba ya mafuta ili kumlaki Bwana arusi!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kwenda kumlaki Bwana arusi, huku wakiwa na akiba ya mafuta yatakayotumika kuwashia taa; ukuaji wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku pamoja na kuwa na maandalizi makini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya viongozi wa Kanisa 154 waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2017- 2018 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kuna Makardinali tisa kati yao ni Kardinali Jean- Louis Tauran, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Kutoka Barani Afrika, Kanisa linawakumbuka kwa namna ya pekee Maaskofu 13. Kutoka Afrika Mashariki na Kati ni Maaskofu 6. Wote hawa wamekumbukwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 3 Novemba 2018 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kwenda kumlaki Bwana arusi, huku wakiwa na akiba ya mafuta yatakayotumika kuwashia taa; ukuaji wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku pamoja na kuwa na maandalizi makini! Wito na maisha ya Kikristo, daima ni mwaliko wa kutoka, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, daima waamini ni wasafiri hadi dakika ya mwisho!

Maandiko Matakatifu yanasema, safari hii ni mwaliko wa kwenda kukutana na Bwana arusi, Kristo Yesu aliyelipenda Kanisa lake upeo, kiasi hata cha kujisadaka, ili kuwaangazia njia wale wanaomfuasa, changamoto ni kuendelea kukua na kukomaa katika upendo wa kukutana na Bwana arusi, kilele cha maandalizi yote! Moyo uliosheheni mapendo unaweza kuwasaidia viongozi wa Kanisa kukaza macho yao kwa vile visivyoonekana; ili kuambata mambo msingi katika maisha, tayari kusikiliza sauti ya Kristo, anayekuja kuwaletea chachu ya mageuzi ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, mafuta ya akiba yaliyohifadhiwa kwenye chombo kidogo ni muhimu zaidi kuliko hata vazi la arusi na taa zenyewe, kwani Mwenyezi Mungu anaangalia yale yaliyofichika mioyoni na wala si heshima, nguvu na madaraka; utukufu na mwonekano wa nje; mambo ambayo yanapita na kutoweka kama ndoto ya mchana! Waamini wajitahidi kuboresha maisha yao ya ndani na kamwe wasipende kuonekana kwa nje. Toba na wongofu wa ndani, usaidie mchakato wa kuyatakatifuza maisha ya ndani, ili yaweze kumpendeza Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka bila ya kujibakiza katika toba na wongofu wa ndani, ili kuwa mwanga angavu unaosimikwa katika huduma, kwani falsafa ya kuishi ni huduma. Huduma makini ndio utambulisho unaomwezesha mwamini kuingia katika Karamu ya Mwanakondoo wa Mungu. Jambo la msingi kutambua ni kwa kiasi gani, kama viongozi wameweza kujisadaka bila ya kujibakiza ili kulipa gharama ya upendo wa Mungu. Upendo wa dhati ni maisha yanaosimikwa katika huduma inayopaswa kushuhudiwa na kutolewa sadaka pasi na uchoyo wala ubinafsi!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujiandaa kikamilifu ili kwenda kumpokea Bwana arusi, jambo linalotekelezwa kila siku ya maisha kwa kurutubishwa na upendo, daima wakijitahidi kuipyaisha upendo kwa Kristo na Kanisa lake, ili taa ya huduma iendelee kuwaka! Taa hii inaweza kuzimika, ikiwa kama hakuna jitihada za makusudi za kuendelea kuwekeza katika upendo na badala yake watu kuanza kubweteka katika: faraja na mazoea bila ya kutaka kujisadaka zaidi kwa ajili ya Bwana arusi!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, Kanisa linapowakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia wakiwa na tumaini la ufufuko; kuiga mifano bora ya wale ambao wametekeleza utume wao katika hali ya ukimya, wakahudumia kwa ari na moyo mkuu; wakajiandaa kikamilifu ili kukutana na Bwana arusi; wawe ni mifano bora ya kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa na mwono wa mbali zaidi, daima wakijitahidi kukuza na kudumisha ile hamu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya upendo, tayari kukutana na Bwana arusi!

Papa: Makardinali
03 November 2018, 15:07