Vatican News
Papa Francisko awapongeza wanawake wanaojitosa kufanya tafiti na kufundisha taalimungu! Papa Francisko awapongeza wanawake wanaojitosa kufanya tafiti na kufundisha taalimungu!  (Vatican Media)

Papa Francisko awapongeza wanawake wanaojitosa katika tafiti za ufundishaji wa taalimungu!

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wanawake wanaoendelea kujipambanua katika tafiti na ufundishaji wa taalimungu kama ilivyo kwa Professa Mariane Schlosser na Professa Anne-marie Pelletier na kwamba, mchango wa wanawake katika tafiti za kitaalimungu kisayansi na ufundishaji wake zinapaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 15-16 Novemba 2018 wamefanya kongamano la kimataifa lililojadili kuhusu: uhuru wa kidini, haki asilia, mabadiliko katika uhuru na utamaduni wa haki msingi za binadamu pamoja na upotoshwaji wa dhana hizi katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kutoa Tuzo ya Ratzinger kwa Professa Mariane Schlosser na Msanifu majengo Mario Botta walioshinda tuzo hii kwa mwaka 2018.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake wakati wa kutoa Tuzo ya Ratzinger ameungana na viongozi, marafiki pamoja na wadau mbali mbali wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kutokana na amana na urithi mkubwa wa kitamaduni na maisha ya kiroho kutoka kwake, mambo yanayopaswa kuendelezwa na kudumishwa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tangu ujana wake alijihusisha kikamilifu katika masuala ya kitaalimungu na matunda ya kazi zake, yanajionesha kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; katika maisha na wito wake kama Padre, Askofu, Kardinali na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki.

Kardinali Joseph Ratzinger, aliona matatizo na changamoto za ulimwengu mamboleo, akalitaka Kanisa kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu na Mapokeo Hai ya Kanisa kama chachu ya majadiliano na tamaduni mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wasomi na wanazuoni kuendelea kufanya tafiti katika machapisho ya Papa Mstaafu Benedikto XVI kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo mintarafu imani ya Kanisa, ili kukoleza majadiliano katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wanawake wanaoendelea kujipambanua katika tafiti na ufundishaji wa taalimungu kama ilivyo kwa Professa Mariane Schlosser na Professa Anne-marie Pelletier  na kwamba, mchango wa wanawake katika tafiti za kitaalimungu kisayansi na ufundishaji wake zinapaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Paulo VI alitambua na kuthamini mchango wa Mtakatifu Theresa wa Avilla na Catharina wa Siena na wengine kama Mtakatifu Theresa wa Lisieux na Ildegarda wa Bingen nao wakatambuliwa na viongozi wa Kanisa kutokana na mchango wao kwa Kanisa.

Baba Mtakatifu amempongeza pia Msanifu majengo Mario Botta kwa kudadavua historia ya sanaa ya majengo ya Kanisa kama kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, chachu ya Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni historia ambayo imefafanua imani ya jumuiya inayoamini na kujikita katika maisha ya sala, ili kujenga mji wa watu wa Mungu. Huu ni mchango mkubwa unaopaswa kutambuliwa na kuenziwa na Kanisa, kwa kuendelea kujikita katika mwono wa maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha maeneo ya hadhara kama sehemu za kukuza utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa kusema, changamoto za mipango miji katika ulimwengu mamboleo zinaweza kushughulikiwa kwa mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu: chemchemi ya nguvu, furaha na matumaini. Matumaini ni kati ya tema ambazo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alizipenda sana katika maisha na utume wake kama yanavyofafanuliwa na Mtakatifu Bonaventura.

Papa: Tuzo Ratzinger
17 November 2018, 15:26