Tafuta

Vatican News
Tarehe 2 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote! Tarehe 2 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote!  (ANSA)

Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote!

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 2 Novemba, kila mwaka, Mama Kanisa anawakumbuka Waamini Marehemu Wote. Papa Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Laurentino yaliyoko mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Siku kuu ya Watakatifu Wote, tarehe Mosi Novemba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amechukua fursa hii kuwasalimia na kuwatakia heri na baraka mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia, waliohudhuria Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa namna ya pekee kabisa, amewashukuru wale wote walioshiriki katika shindano la “Mbio za Watakatifu” yaliyoandaliwa na Mfuko wa “Utume wa Don Bosco”, kwa kushiriki kwa furaha katika maadhimisho haya. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa mkakati na uwepo wao.

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 2 Novemba, kila mwaka, Mama Kanisa anawakumbuka waamini marehemu wote. Papa Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Laurentino yaliyoko mjini Roma. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza kwa njia ya sala katika maadhimisho ya siku hii maalum iliyotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani na sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani. Mwishoni, amewatakia waamini na mahujaji wote, Siku kuu njema ya Watakatifu wote!

Marehemu Wote
01 November 2018, 16:01