Papa Francisko: Madhabahu ni mahali pa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo! Papa Francisko: Madhabahu ni mahali pa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo! 

Madhabahu ni mahali pa ushuhuda wa imani, mapendo na matumaini!

Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, kuanzia tarehe 27-29 Novemba 2018, limekuwa na Kongamano la Kimataifa kuhusu madhabahu lililokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya”. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 29 Novemba 2018 amekutana na wajumbe wa kongamano hili na kukazia umuhimu wa ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao!

Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa na kuthaminiwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao!

Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliokata tamaa na kwamba, Mama huyu anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: neema na rehema pamoja na kuzidimisha upendo kwa Mungu na jirani!

Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!

Papa: Madhabahu

 

29 November 2018, 16:28