Tafuta

Tarehe 9 Novemba ni Siku kuu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano Tarehe 9 Novemba ni Siku kuu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano 

Miili yenu ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu!

Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni na kichwa cha Makanisa yote ya Jimbo kuu la Roma lililowekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 7 Novemba 2018 wakati wa Katekesi yake amekumbusha kwamba, tarehe 9 Novemba 2018, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Kanisa hili ni Mama ya Makanisa yote ulimwenguni na kichwa cha Makanisa yote ya Jimbo kuu la Roma lililowekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Mkombozi wa dunia. Baadaye, liliwekwa pia chini ya ulinzi wa Yohane Mbatizaji na Mwinjili Yohane. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini, uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini na imani yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. 

Hili lilikuwa ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbali mbali. Kanisa hili ni kielelezo cha Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Ni alama ya upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko, ambaye, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambaye, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu, kumbe hii pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dhambi!

Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo mwenyewe. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya watu wanaoishi nao, kwa kudumisha umoja na udugu unaotengeneza sadaka safi inayompendeza Mungu. Waamini wanahimizwa kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kitamaduni na kihistoria pamoja na kutambua kwamba, hata wao wenyewe miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kanisa kuu la Laterano
09 November 2018, 10:15