Tafuta

Vatican News
Tarehe 2 Novemba Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote! Tarehe 2 Novemba Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote!  (Vatican Media)

Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote: Heri za mlimani!

Papa Francisko tarehe 2 Novemba 2018, ametembelea na kusali kwenye makaburi ya watoto wadogo waliofariki dunia kutokana na magonjwa, ajali na wale ambao wametolewa mimba hata kabla ya kuzaliwa! Baadaye, Baba Mtakatifu ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Laurentino yaliyoko nje kidogo ya mji wa Roma na hatimaye kutembelea Makanuri ya Mapapa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu wote, iliyoadhimisha na Mama Kanisa, tarehe 2 Novemba 2018, ametembelea na kusali kwenye makaburi ya watoto wadogo waliofariki dunia kutokana na magonjwa, ajali na wale ambao wametolewa mimba hata kabla ya kuzaliwa! Baadaye, Baba Mtakatifu ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Laurentino yaliyoko nje kidogo ya mji wa Roma.

Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kutunza: kumbu kumbu na matumaini mintarafu mwanga wa Heri za Mlimani, ili kutodanganyika katika maisha na mambo mpito! Baba Mtakatifu aliporejea, alikwenda moja kwa moja kwenye Makaburi ya watangulizi wake yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kusali na kuwaombea kwa faragha! Baba Mtakatifu alipowasili moja kwa moja alikwenda kutembelea na kusali kwenye makaburi ya watoto wadogo, amesoma majina yao na ujumbe ulioandikwa kwenye makaburi haya, baadaye, akapata nafasi pia ya kukutana na wazazi waliowapoteza watoto wao wachanga! Machozi ya huruma na mapendo, yaliwabubujika wazazi na walezi hawa walipokutana na Baba Mtakatifu!

Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amekita mahubiri yake kwenye Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu! Amekazia kuhusu kumbu kumbu ya maisha yaliyopita, yaliyopo na yale ya mbeleni! Baba Mtakatifu anasema, si rahisi sana kufanya kumbu kumbu, lakini ni muhimu sana katika historia na maisha ya watu, kwani kumbu kumbu inawajenga na kuwaimarisha watu, kwa kujisikia kwamba, wamekita miguu yao katika historia na maisha ya watu!

Kumbu kumbu inawasaidia waamini kuwatambua na kuwakumbuka wale waliowatangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko! Hii ni kumbu kumbu ya umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki kikamilifu katika hija ya maisha, lakini leo hii hawapo tena! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi kufanya kumbu kumbu, ili kupitia yaliyotendeka katika maisha, familia, jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Lakini, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote, ili kuwasaidia waamini kutambua historia na asili ya ndugu zao katika Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kumbu kumbu hii inasimikwa katika matumaini yanayowawezesha watu kukutana na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aliyewakirimia zawadi ya maisha. Haya ni matumaini yanayobubujika kutoka Yerusalemu ya mbinguni, kielelezo cha: uzuri na upendo mkuu ambao Bwana arusi anautoa kwa bibi arusi, “asali wa moyo wake”. Kumbe, kumbu kumbu na matumaini yawawezeshe waamini kukutana na Mwenyezi Mungu, Muumbaji na Mkombozi, ambaye daima anawasubiri watu wake.

Mwanga wa Heri za Mlimani ni dira na mwongozo katika safari ya maisha ya kiroho, unaomwezesha mwamini kuona na hatimaye, kupitia njia salama! Heri hizi ni: huzuni, upole, njaa na kiu ya haki, rehema, moyo safi, utapanishi na udhia kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Katika Makaburi la Laurentino, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu katika maisha: Kumbu kumbu angavu na endelevu, matumaini ambayo Mama Kanisa anaadhimisha katika imani juu ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele njia inayowaelekeza waamini katika upendo mkamilifu.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia paji la kumbu kumbu, kama mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Mwenyezi Mungu awakirimie waja wake zawadi ya matumaini, ili kuwa na ari na mwamko wa kuangalia ya mbeleni, ili hatimaye, kuufikia upendo mkamilifu ambao ni Mungu mwenyewe!

Papa: Marehemu Wote
03 November 2018, 14:44