Papa Francisko anawaalika waamini kuendelea kujiandaa kumpokea Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na Sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma! Papa Francisko anawaalika waamini kuendelea kujiandaa kumpokea Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na Sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma! 

Papa Francisko: Jiandaeni kukutana na Kristo katika: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo ya huruma!

Mama Kanisa anapohitimisha Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, anawaalika watoto wake kujiandaa kikamilifu ili kuanza hija ya kumwendea, ili hatimaye, waweze kukutana na Kristo Yesu anayezima kiu na njaa ya maisha yao ya ndani kwa njia ya: maadhimisho na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; Maisha ya Sala na Upendo kwa Mungu na jirani unaomwilishwa katika matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 28 Novemba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Mama Kanisa anapohitimisha Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, anawaalika watoto wake kujiandaa kikamilifu ili kuanza hija ya kumwendea, ili hatimaye, waweze kukutana na Kristo Yesu anayezima kiu na njaa ya maisha yao ya ndani kwa njia ya: maadhimisho na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; Maisha ya Sala na Upendo kwa Mungu na jirani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo makini cha wafuasi wa Kristo na kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu amendelea kufafanua kwamba, Jumapili ijayo tarehe 2 Desemba 2018, Kanisa litaanza Kipindi cha Majilio, kama sehemu ya maandalizi ya kukutana na hatimaye, kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa tena katika sakafu ya maisha yao. Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu anakuja kukutana na binadamu, hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, maskini, wahitaji na waathirika wa vita inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao, na hatimaye, kuwakirimia maisha mapya, yaani kwa kuzima kiu ya Mungu ili waweze kumpenda na kupendwa naye! Amewatakia waamini na mahujaji wote furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Amewataka waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Roho Mtakatifu kwa jirani zao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameishukuru familia ya Mungu kutoka Lithuania ambayo alipata bahati ya kuitembelea hivi karibuni na kuonja ukarimu wake. Kwa mara nyingine tena ameitaka kuonesha ujasiri katika imani, matumaini na mapendo mambo muhimu sana katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Papa: Mwaka wa Kanisa

 

 

 

 

 

28 November 2018, 15:38