Amri za Mungu ni tafakari ya Uso wa Kristo ili kumpokea Roho Mtakatifu anayewakirimia matunda yake! Amri za Mungu ni tafakari ya Uso wa Kristo ili kumpokea Roho Mtakatifu anayewakirimia matunda yake! 

Papa Francisko: Amri za Mungu: Ni tafakari ya Uso wa Kristo ili kupokea Matunda ya Roho Mtakatifu!

Tafakari ya maisha katika mwanga wa Amri za Mungu unamwonesha mwamini kuwa ni mtu wa shukrani, huru, mkweli, anayebariki, mkomavu, mlinzi na mtunza Injili ya uhai; mwaminifu, mkarimu na mkweli; mambo ambayo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake ya kila siku na hivyo kujiona kuwa mbele ya Kristo Yesu, kila siku ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wagalatia, anawaalika Wakristo kuenenda kwa Roho, kwani hawatazitimiza kamwe tamaa za mwili, kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho na Roho hushindana na mwili! Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo yote haya hakuna Sheria! Tamaa ya mwili ni mchakato ambao umeongoza tafakari ya kina wakati wa katekesi za Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Amri za Mungu, mintarafu ufunuo wa mwanga wa Kristo Yesu.

Hii ni sehemu ya Katekesi kuhusu Amri za Mungu kama ilivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI, mjini Vatican, Jumatano, tarehe 28 Novemba 2018. Baba Mtakatifu anasema, moyo wa shukrani ni msingi wa imani na utii kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemkirimia mwanadamu yote na kwamba, anamtaka kumwabudu Muumba wake peke yake badala ya kuabudu “miungu wa kuchongwa”. Hawa ni miungu wanaomtumbukiza mwamini katika utumwa badala ya kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, aliyewawezesha kuwa waana wa Baba wa milele! Huu ni mchakato wa baraka na ukombozi; kwani mwamini anatambua kwamba, Mungu peke yake ndiye mwamba na wokovu wake, hatatikisika kamwe.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio muhtasari wa historia ya maisha ya kila mwamini inayoleta upatanisho na ulinganifu tangu utoto hadi katika maisha ya utu uzima, ili kutoa uzito katika ukweli na kwa watu wanaowazunguka! Ni katika mwelekeo huu, waamini wanaunda uhusiano na jirani kwa kujikita katika upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, upendo ambao umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutambua uzuri unaofumbatwa katika uaminifu, ukarimu na ukweli wa maisha, hali ambayo inahitaji moyo mpya, ambao ni Hekalu la Roho Mtakatifu, kwa kutamani mambo ya maisha ya kiroho, ambayo yanapatikana kwa njia ya neema na kwa namna ya pekee, kwa njia ya Amri za Mungu ambazo zimepata utimilifu wake katika maisha na mafundisho ya Yesu, kama alivyoyafafua kwenye Heri za Mlimani!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tafakari ya maisha katika mwanga wa Amri za Mungu unamwonesha mwamini kuwa ni mtu wa shukrani, huru, mkweli, anayebariki, mkomavu, mlinzi na mtunza Injili ya uhai; mwaminifu, mkarimu na mkweli; mambo ambayo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake ya kila siku na hivyo kujiona kuwa mbele ya Kristo Yesu, kila siku ya maisha! Amri za Mungu ni sura na chapa ya Kristo Yesu kama inavyojionesha katika Sanda Takatifu.

Ni kwa njia hii, Roho Mtakatifu anawakirimia waamini Matunda ya Roho Mtakatifu, ili kuenenda katika Roho, ili hatimaye kuona: uzuri, wema na ukweli unaofumbatwa katika maisha ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, waamini wanakirimiwa fadhila ya matumaini, imani na upendo! Ikumbukwe kwamba, ujio wa Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria na kwa njia ya Matunda ya Roho Mtakatifu, waamini wanapata Sheria mpya inayowaongoza katika Roho, kwani kwa njia ya Roho Mtakatifu wanakuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Kristo Yesu anawapenda watu wake, anajitaabisha kuwatafuta, kuwasamehe, kuwafariji pale wanapohuzunika na kupondeka moyo!

Kristo Yesu anawaunganisha na upendo wa Baba wa milele! Kumbe, hapa kinachopewa mkazo anasema Baba Mtakatifu ni upendo kwa Mungu na jirani na kuwaachia wengine nafasi ya kuonja upendo huu, kama kielelezo makini cha utimilifu wa Sheria ulioletwa na Kristo Yesu! Ni katika muktadha huu, Amri za Mungu zinakuwa ni ukweli mfunuliwa unaokita mizizi yake katika maisha ya mwamini yanayofumbatwa katika upendo, hamu ya kutenda mema, kiu ya kufurahia maisha; hamu ya kupata amani, wema, uzuri, unyenyekevu pamoja na kuwa na kiasi katika maisha!

Kristo Yesu anajibidisha kuwatafuta waja wake, ili kutaka kuzima kiu inayotoka vilindini mwa Mwenyezi Mungu, anayewatamani! Mwenyezi Mungu anawaonea kiu waja wake, ili hatimaye, wao pia wamwonee kiu Yeye! Roho Mtakatifu anawakirimia waamini kiu ya kutenda mema na kuenenda katika upya wa maisha! Kwa wale waliozaliwa upya, hawapaswi kutenda dhambi, kwani wanaenenda katika upya wa maisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, chemchemi ya furaha, upendo. Hii ndiyo maana halisi ya Amri za Mungu yaani: kutafakari Uso wa Kristo, ili aweze kuwafunulia Moyo wake Mtakatifu, hatimaye, kuweza kumpokea Roho Mtakatifu anayewakirimia Matunda yake!

Amri za Mungu

 

 

28 November 2018, 16:08