Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Kardinali Angelo De Donatis wakati wa kufungua mwaka wa masomo 2018-2019. Ujumbe wa Papa Francisko kwa Kardinali Angelo De Donatis wakati wa kufungua mwaka wa masomo 2018-2019. 

Papa Francisko: Mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani!

Kanisa mintarafu mwanga wa Injili linawajibika kushiriki katika mchakato wa amani duniani unaopaswa kusimikwa katika dhana ya kusikiliza na kufahamiana; kwa kukazia na kujikita katika amana na tunu msingi za maisha ya kiutu ili kubomolea mbali utengano na matumizi mabaya ya madaraka yanayopelekea vita na maafa kwa watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano kilichoko mjini Roma, Jumatatu, tarehe 12 Novemba 2018 kimefungua rasmi mwaka wa masomo wa 246 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni tukio ambalo limepambwa kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kardinali Angelo De Donatis, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano; hotuba ya Askofu Marcello Semeraro, Katibu mkuu wa Baraza la Makardinali Washauri ambaye amepembua muswada wa Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Mkahubiri Injili” inayohusu mchakato wa mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Sekretarieti kuu ya Vatican.

Mwongozo wa malezi katika sayansi ya amani ni mada ambayo imepembuliwa na Askofu mkuu Edgar Pena Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican pamoja na kugusia Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyotolewa hivi karibuni na Papa Francisko ambamo anatoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa katika sekta ya elimu, kwani lengo ni kujenga na kukuza umoja na udugu, upendo na mshikamano, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza! Ufunguzi wa mwaka wa masomo 2018-2019 umehitimishwa na Professa Vincenzo Buonomo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Kipapa cha Laterano.

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali Angelo De Donatis amekazia umuhimu wa mchakato wa amani unaofumbatwa katika majadiliano yatakayozima: chuki, uhasama, ubinafsi, hali ya watu kutaka kujikweza; uchu wa mali na madaraka; mambo yanayowanyanyasa na kuwagandamiza maskini! Kusikiliza na kuelewana; mchango wa Kanisa katika kudumisha amani na kwamba, vyuo vikuu ni majukwaa ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu!

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa mintarafu mwanga wa Injili linawajibika kushiriki katika mchakato wa amani duniani unaopaswa kusimikwa katika dhana ya kusikiliza na kufahamiana; kwa kukazia na kujikita katika amana na tunu msingi za maisha ya kiutu ili kubomolea mbali utengano na matumizi mabaya ya madaraka yanayopelekea vita na maafa kwa watu na mali zao. Upatanisho, haki na amani; maendeleo endelevu na fungamani; ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya mambo yanayoweza kuchochea misingi ya amani na huduma kwa ajili ya watu.

Kanisa anasema Baba Mtakatifu, halina budi kujielekeza zaidi katika upatanisho, kwa kutafuta suluhu ya matatizo yanayoathiri amani, mafungamano ya kijamii, matatizo ya ardhi; kwa kusimama kidete kutetea uhai pamoja na haki msingi za binadamu na kiraia. Hii ni dhamana inayotekelezwa pia na Vatican kwa njia za kidiplomasia, ili kuvunjilia mbali kinzani kwa kuheshimu haki msingi za binadamu, maendeleo endelevu na fungamani ya watu na nchi zao!

Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, ni vyombo vya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, vinavyopaswa kuendelea kuboreka na kujipyaisha ili kukidhi mahitaji ya nyakati. Vyuo vikuu vya Kikatoliki vinaweza kuwa ni chachu, chumvi na mwanga wa Injili ya Kristo na Mapokeo hai ya Kanisa kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo, ili kuliwezesha Kanisa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari. Changamoto hii inaweza kutekelezwa kwa kutangaza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; bila woga kwa kuthubu kutafuta amani kwa watu na mataifa yote!

Baba Mtakatifu anakitaka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano kuanzisha mchepuo wa Sayansi ya Amani, itakayoshirikisha vitivo vya: taalimungu, falsafa, sheria, uchumi na masuala ya kijamii, ili kujenga mwingiliano wa vitivo, ili hatimaye, wafunzi wanapohitimu waweze kujipatia shahada ya kwanza pamoja na shahada ya uzamili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Chuo Kikuu cha Laterano kitalishughulikia ombi ili kutoa majiundo makini kwa wakleri, watawa na waamini walei sayansi ya amani, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani.

Jumuiya hii pia ijisikie kuwa na wajibu wa kupandikiza mbegu ya utamaduni wa amani kwa: kusikiliza, kwa kudumisha weledi, sadaka na majitoleo na yote haya , daima yafanyike katika unyenyekevu, upendo na utashi wa kuwa yote kwa ajili ya wote! Watakatifu Yohane XXIII na Paulo VI miamba wa amani, walioachangia kwa kiasi kikubwa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika dhana ya amani, wawalinde na kuwaombea wote!

Papa: Ujumbe: Chuo Kikuu
12 November 2018, 14:13