Tafuta

Kanisa linajiandaa kuadhimisha mkutano maalum kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo kuanzia tarehe 21- 24 Fabruari 2019 Kanisa linajiandaa kuadhimisha mkutano maalum kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo kuanzia tarehe 21- 24 Fabruari 2019 

Papa Francisko aunda Kamati kuu ya maandalizi ya mkutano dhidi ya watoto wadogo

Kamati hii inaundwa na Kardinali Blase J. Cupich na Kardinali Oswald Gracias; wengine ni Askofu mkuu Charles Jude Scicluna, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mbinu mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia unapania pia kuliwezesha Kanisa kujitakatifuza kwa kujikita katika maadili na utu wema, changamoto inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye ameunda Kamati kuu itakayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Kamati hii inaundwa na Kardinali Blase J. Cupich na Kardinali Oswald Gracias; wengine ni Askofu mkuu Charles Jude Scicluna, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Kamati kuu itawashirikisha wakuu wa Makanisa ya Mashariki pamoja na viongozi wakuu kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican, chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, huu ni mkutano utakaohudhuriwa na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na wawakilishi wa wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, ulinzi na tunza ya watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuwasaidia viongozi wa Kanisa kuona madhara ya nyanyaso za kijinsia katika maisha, utume, utu na heshima ya watoto hawa. Walengwa wakuu wa mkutano huu ni Maaskofu ambao wanaowajibu mkubwa wa kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto wadogo. Wataalam waliobobea katika sakata hili wamealikwa ili kuchangia sera na mbinu mkakati utakaotumiwa ili Kanisa liweze kuwajibika katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu!

Kardinali Seàn Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM, iliyoundwa mwezi Machi 2014 na Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia ni vitendo ambavyo kamwe haviwezi kukubalika kimaadili na ikiwa kama vitendo hivi vinafanywa na watu wenye dhamana katika uongozi wa Kanisa. Ni vitendo vinavyokera na kuudhi sana, kwani vinakwenda kinyume kabisa cha dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kashfa kama hizi zinapotokea ndani ya Kanisa, haitoshi tu kwa wahusika kuomba radhi, bali Kanisa linapaswa kuchukua hatua za kinidhamu mara moja, ili kuhakikisha kwamba, kashfa za namna hii hazijirudii tena ndani ya Kanisa.

Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuonesha mshikamano na wahanga wa vitendo hivyo pamoja na kuwatendea haki, ili kwamba, watoto wanaotafuta majiundo makini na fungamani katika maeneo ya Kanisa wanakulia katika mazingira bora na salama. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Kanisa limejifunza kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kujisafisha na kujitakatifuza ili kuwahakikishia watoto na vijana usalama wa maisha yao wanapokuwa katika maeneo yanayolizunguka Kanisa.

Kardinali Seàn Patrick O’Malley anakaza kusema, wakati huu Mama Kanisa anapofanya hija ya toba na wongofu wa kimisionari, ni matumaini yake kwamba, Maaskofu mahalia wataendelea kujipanga kikamilifu, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linawaundia watoto mazingira salama na yenye amani katika malezi na makuzi yao. Huu ni wakati wa kutenda kwa kuzingatia ukweli na uwazi; kwa kuwawajibisha wahusika pamoja na Kanisa kuendelea kushirikiana na serikali mbali mbali katika kudhibiti vitendo hivi vya aibu. Waathirika wa vitendo hivi wasaidiwe kuganga na kuponya madonda yao ya ndani! Mapambano haya yanahitaji ushirikiano mwema kati ya wakleri, watawa na waamini walei ili kukabiliana na janga hili ambalo limekuwa ni “mwiba mkali” katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian anasema, mkutano wa Februari ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, unapaswa kuandaliwa vyema, kama jukwaa la sala, tafakari, toba na wongofu wa ndani tayari kuibua mbinu mkakati utakaotumiwa na Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Mkutano huu unaweza kuangaliwa kama safari ya viongozi wa Kanisa kutembea kwa pamoja kama Sinodi, dhana inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mkutano utakaopmbeua kwa kina na mapana kashfa ya nyanyaso za kijinsia; ufahamu na aibu ya Kanisa; toba na wongofu wa ndani; sala na mang’amuzi, na hatimaye, Kanisa kufanya maamuzi magumu yanayofumbatwa katika haki na kweli!

Kamati Kuu: Watoto

 

24 November 2018, 14:45