Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akumbuka mauaji ya holodomor miaka 85 iliyopita, aombea amani nchini Ukraine. Papa Francisko akumbuka mauaji ya holodomor miaka 85 iliyopita, aombea amani nchini Ukraine. 

Papa Francisko akumbuka mateso ya wananchi wa Ukraine, aombea amani!

“Holodomor” maana yake, mauaji ya watu kwa njaa yaliyobuniwa na kutekelezwa na utawala wa Kikomunisti, uliowataka wananchi kutoa mazao na nafaka zote kwa serikali. Mauaji haya ya kutisha yalifanyika kunako mwaka 1929 hadi mwaka 1933 na kutambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu wote, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 25 Novemba 2018, amesali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine, ambayo, Jumamosi, tarehe 24 Novemba 2018 imefanya kumbu kumbu ya Miaka 85 tangu yalipotokea mauaji ya Holodomor.

Familia ya Mungu nchini Ukraine imefanya kumbu kumbu hii kwa sala na makesha, huku ikikumbuka jinsi ambavyo watu waliteseka sana wakati wa mauaji ya “Holodomor” maana yake, mauaji ya watu kwa njaa yaliyobuniwa na kutekelezwa na utawala wa Kikomunisti, uliowataka wananchi kutoa mazao na nafaka zote kwa serikali. Mauaji haya ya kutisha yalifanyika kunako mwaka 1929 hadi mwaka 1933 na kutambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Takwimu zinaonesha kwamba, watu milioni tano walipoteza maisha kwa kufa kwa baa la njaa, wengine wakapelekwa uhamishoni na wale waliosalia wakateswa na kunyanyaswa sana. Baba Mtakatifu amelikumbuka tukio hili, lakini zaidi, anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine ambayo tangu mwaka 2014 imegeuka kuwa ni uwanja wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Matukio kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko, yasijirudie kamwe katika historia ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa washiriki wa kongamano kuhusu “Uzazi” lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Papa: Ukraine

 

25 November 2018, 08:25