Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sanaa na vivutio vya kitamaduni visaidie huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi! Papa Francisko: Sanaa na vivutio vya kitamaduni visaidie huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi!  (ANSA)

Papa Francisko: Sanaa na vivutio vya kitamaduni visaidie huduma kwa maskini!

Mapato na faida inayopatikana kutokana na sanaa na vivutio vya kitamaduni yanapaswa kutumika kugharimia shughuli na huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na  Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kwa muda wa siku mbili yaani kuanzia tarehe 29-30 Novemba 2018 wamekuwa wakiendesha kongamano kuhusu “Usitishwaji wa huduma ya kiroho katika maeneo ya ibada pamoja na utunzaji makini wa vivutio vya kitamaduni vinavyomilikiwa na Kanisa”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza al Kipapa la Utamaduni amekazia umuhimu wa utunzaji wa nyaraka za Kanisa, maeneo ya ibada na vivutio vya kitamaduni vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa!

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe kutambua, kuthamini na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho, tayari kuzipokea na kuzimwilisha katika upya wa kiinjili, tayari kushiriki katika utunzaji bora wa mazingira, ambayo kimsingi ni kielelezo cha hali ya juu cha kazi ya uumbaji. Kumbe, kazi za usanifu majengo wenye mvuto na ubunifu, maboresho ya makazi ya watu sanjari na ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi ambayo Mama Kanisa anapenda kuyapatia umuhimu wa pekee katika maisha na utume wake.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, mambo ya sanaa ni kielelezo cha hali ya juu cha maarifa ya binadamu yanayoonesha na kukuza sifa ya uzuri, ukuu na utakatifu wa Mungu. Ndiyo maana sanaa inapewa nafasi ya pekee katika Kanisa kwani zinasaidia kukuza imani, uchaji, kanuni na Mapokeo. Sanaa takatifu ni kielelezo cha cha imani ya jumuiya ya waamini, ni chombo cha uinjilishaji, mahubiri na katekesi inayotumika kama sehemu ya majiundo endelevu na makini kwa ajili ua watu wa Mungu.

Mapato na faida inayopatikana kutokana na sanaa na vivutio vya kitamaduni yanapaswa kutumika kugharimia shughuli na huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Laurenti, Shemasi anakumbukwa sana kutokana na ujasiri wake, kwa kuuza baadhi ya sanaa na malikale ya Kanisa ili kuwahudumia maskini! Kumbe, utunzaji wa sanaa na vivutio vya kitamaduni ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, lakini zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya Makanisa ambayo kutokana na sababu mbali mbali hayawezi tena kutumika kama nyumba za Ibada, changamoto kwa familia ya Mungu katika maeneo na mazingira kama haya ni kujaribu kukubali mvutano kati ya utimilifu na upungufu na kutoa nafasi kwa wakati pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Hii ni changamoto ambayo tayari imekwishafanyiwa tafakari na Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia na utekelezaji wake umekwisha anza. Hii ndiyo changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatoa hata kwa washiriki wa kongamano hili, ili kuibua mbinu mkakati utakaowasaidia Maaskofu kufanya maamuzi ya kina, kwa kuwashirikisha watu wa Mungu na serikali husika.

Usitishwaji wa huduma ya Makanisa kuwa nyumba za ibada iwe ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa shughuli za kichungaji, kwa kuwapatia watu taarifa kamili na matokeo yake yaweze kuridhiwa na wengi! Makanisa yasishughulikiwe kwa mwono wa kiuchumi na kitekonolojia tu, bali yaangaliwe katika mwanga wa kinabii, kama urithi wa imani ya Kanisa inayompokea na kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo, Bwana wa historia!

Kongamano Mali ya Kanisa

 

 

 

30 November 2018, 16:05