Tafuta

Papa Francisko anaipongeza Jumuiya ya Kiekumene ya Bose kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Papa Francisko anaipongeza Jumuiya ya Kiekumene ya Bose kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Bose: Imani, umoja na udugu

Jumuiya ya Kiekumene ya Bose, imekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya Wakristo wa Makanisa mbali mbali kiasi cha kuwa ni jukwaa la maisha ya sala, mahali pa kukutanikia na kujadiliana; mahali pa kuimarisha na kudumisha imani, umoja na mapendo kadiri ya utashi wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 11 Novemba 1968 Fra Enzo Bianchi akishirikiana na ndugu zake wachache, walianzisha Jumuiya ya Kiekumene ya Bose iliyobahatika kuonja wema na ukarimu kutoka kwa majirani pamoja na viongozi wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mintarafu majadiliano ya kiekumene. Kunako mwaka 1971, Katiba ya Jumuiya hii ikapitishwa rasmi na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Jumuiya hii sehemu mbali mbali za dunia, mahali ambapo waamini wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo wanashirikiana kukoleza majadiliano ya kiekumene.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kiekumene ya Bose yamepambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu na ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Katika ujumbe, Baba Mtakatifu anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya maisha ya kijumuiya, matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; chachu ya upyaisho wa maisha ya kitawa mintarafu mwanga wa Injili unaofumbatwa katika mapokeo ya kimonaki.

Jumuiya ya Kiekumene ya Bose, imekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya Wakristo wa Makanisa mbali mbali kiasi cha kuwa ni jukwaa la maisha ya sala, mahali pa kukutanikia na kujadiliana; mahali pa kuimarisha na kudumisha imani, umoja na mapendo kadiri ya utashi wa Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja! Baba Mtakatifu anaipongeza Jumuiya hii kwa moyo wake wa ukarimu kwa watu wote; utamaduni wa usikivu kwa wale wote wanaotafuta maana ya maisha, amani na utulivu wa ndani. Jumuiya hii imekuwa ni mahali pa vijana kufanyia mang’amuzi ya miito yao katika maisha, ili hatimaye, waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao vyema. Matunda ya kazi hii ya imani na upendo ni mengi kiasi kwamba si rahisi sana kuyataja, lakini yanajulikana bayana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka wanajumuiya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Iwe ni Jumuiya ambamo wazee na vijana wanasaidiana na kukamilishana katika hekima na udumifu, bila kuwasahau maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Bose, kuwa na jicho la pekee kwa watoto wadogo, maskini, mahujaji na wageni, kwani wao pia ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kiekumene ya Bose yawe ni kipindi cha neema, fursa ya kutafakari kwa kina na mapana juu ya wito na utume wao, tayari kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaimarisha na kuwapatia ujasiri wa kusonga mbele katika hija ya maisha yao ya kiroho, kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita, kwa kuendelea kukita maisha yao katika Injili, maisha ya kidugu katika upendo, kielelezo cha Jumuiya ya watu wanaoshikamana.

Papa: Bose
13 November 2018, 16:39