Papa Francisko akutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini. Papa Francisko akutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini. 

Papa Francisko: Viongozi wa Kanisa iweni wachungaji wa watu!

Chuo cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini hakina utambulisho wa kitaifa wala karama, bali ni jukwaa la mawasiliano ya watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini; mahali ambapo majandokasisi wanapewa fursa ya kuwa na mwono mpana zaidi, tafakari ya kina na uzoezi wa umoja miongoni mwa watu wa Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chuo cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini kilichoko mjini Roma, kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 160 tangu kuanzishwa kwake kunako tarehe 21 Novemba 1858 na kubahatika kuwafunda majandokasisi 4,222. Kwa wale ambao hawakubahatika kufikia Daraja Takatifu ya Upadre wanaendelea kuwa ni mabalozi wema katika shughuli mbali mbali za maisha ndani na nje ya Kanisa. Kati ya Maaskofu 474 waliosoma katika chuo hiki kuna Makardinali 37 na kwamba, kuna waamini 10 ambao wamo kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa ni watakatifu, matendo makuu ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Jumuiya ya Chuo kikuu hiki, amewataka wakleri kuhakikisha kwamba,  wanafuata mifano bora ya watakatifu kama Mtakatifu Oscar Armulfo Romero: mchungaji mwema, nabii, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu na hatimaye, sasa ni chombo cha upatanisho wa kitaifa. Wakleri wametakiwa kulinda na kudumisha mizizi ya utamaduni na maisha ya kiroho kutoka Amerika ya Kusini, ili kweli waweze kuwa ni wachungaji wa watu wa Mungu na wala si watumishi wa Serikali!

Baba Mtakatifu anasema, Chuo cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini hakina utambulisho wa kitaifa wala karama, bali ni jukwaa la mawasiliano ya watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini; mahali ambapo majandokasisi wanapewa fursa ya kuwa na mwono mpana zaidi, tafakari ya kina na uzoezi wa umoja miongoni mwa watu wa Amerika ya Kusini. Changamoto kubwa kwa sasa mbele yao, ili kulinda na kudumisha tamaduni za watu wao na hivyo kulisaidia Kanisa katika mchakato wa utamadunisho. Amerika ya Kusini, daima imejitambulisha kuwa ni daraja la watu kukutana, lakini wanapaswa kuwa macho na ukoloni wa kiitikadi unaotaka kulivamia hata Kanisa.

Chuo cha Kipapa cha Pio cha Amerika ya Kusini kinapaswa kuwa ni mahali pa kujenga na kukuza mshikamano wa urafiki na udugu; kwa kufahamiana vyema zaidi; kwa kusaidiana wakati wa raha na shida za maisha na kwa pamoja kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuwaandama watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Chuo hiki kiwe ni mahali pa kujenga Jumuiya ya Wakleri inayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu; furaha na matumaini, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini, kwa kutambua kwamba, kwa pamoja wanayo amana ya maisha inayowabidisha kujenga mshikamano kati ya Makanisa na waamini wake; tayari kupandikiza mbegu ya matumaini.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Amerika ya Kusini inapitia kipindi kigumu cha “madonda ya zamani na mapya” yanayohitaji wapatanishi na wajenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: umoja na upendo; katika haki na amani; tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayowaletea watu toba na wongofu wa ndani; kwa kujenga na kudumisha urafiki na mahusiano mema na Kristo Yesu, ili kweli waamini waweze kuondokana na dhana ya Kanisa la Amerika ya Kusini ambalo ni “Mungu pasi na Kanisa; Kanisa pasi na Kristo na Kristo pasi na watu wa Mungu” kielelezo cha upotofu wa imani. Amerika ya Kusini ni mahali ambapo upendo kwa Kristo Yesu umeacha chapa katika akili na nyoyo za watu. Huu ni mwaliko wa kuwa karibu na watu wa Mungu, ili waweze kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa! Wakleri wajenge urafiki mwema na Kristo Yesu pamoja na waamini wao; wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kwa maskini na wadhambi wanaokimbilia ulinzi na tunza ya Baba yao wa milele.

Wakleri watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la Mwili wa Kristo; yaani Kanisa, wajenge na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza na kujibu vyema kilio na matamanio halali ya watu wa Mungu; washikamane na wale wanaolia na kuomboleza; wafurahie maisha na wale wanaofurahi na kumtukuza Mungu, daima wakikumbuka kuwaombea wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi! Mtakatifu Oscar Armulfo Romero awe ni chachu ya utakatifu Amerika ya Kusini, kwa kujikita katika tafakari ya Neno la Mungu na kuguswa na mahangaiko ya watu wao, daima umati wa watakatifu na mashuhuda wa imani wawe ni chachu ya utakatifu, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza!

Katika hija ya utume na maisha ya kiroho, daima wanaye Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayewalinda, anayewaombea na kuwasindikiza katika safari ya maisha yao, huku bondeni kwenye machozi, ili kweli waweze kuwa ni wachungaji wa watu wa Mungu na kamwe si wafanyakazi wa Serikali. Wakleri daima wajitahidi kuwa ni watu wa tafakari inayomwilishwa katika matendo; wawe ni waliovikwa fadhila ya utii na wachapakazi, watu ambao wako tayari kutumwa mahali popote. Wakleri wawe na hekima itakayowawezesha vijana kufanya mang’amuzi ya maisha na wito wao, daima wakijitahidi kumpatia Mwenyezi Mungu sifa na utukufu, kwa kuwahudumia: maskini, wagonjwa pamoja na kuendelea kujifunza katika maisha.

Papa: Amerika ya Kusini
16 November 2018, 15:15