Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewaandikia barua Wafranciskani wanaoishi na kutekeleza utume wao nchini Siria kuwa ni mashuhuda wa imani. Papa Francisko amewaandikia barua Wafranciskani wanaoishi na kutekeleza utume wao nchini Siria kuwa ni mashuhuda wa imani. 

Barua ya Papa Francisko kwa Wafranciskani nchini Siria! Ushuhuda wa imani kwa Kristo!

Mashuhuda wa imani ni kielelezo cha utukufu wa Kanisa na chemchemi ya matumaini ya Wakristo. Ni kutokana na ukweli huu, mashuhuda wa imani na wafiadini wanaendelea kupambana na mawimbi mazito ya bahari katika maisha yao! Kumbe, ushuhuda huu unapaswa kuwa endelevu hata katika nyakati za shida na madhulumu, kwani kwa njia yao, watu wanapata wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Barua Wafranciskani wanaoishi nchini Siria ambayo imegeuka kuwa ni uwanja wa vita kwa miaka ya hivi karibuni. Baba Mtakatifu anatambua mateso na mahangaiko yao na kwamba, yuko karibu pamoja nao kwa njia ya sala na sadaka yake ya kila siku. Maisha yao ni ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Familia ya Mungu nchini Siria inaendelea kupekenyuliwa na umaskini, kielelezo na ushuhuda wa mateso endelevu ya Kristo miongoni mwa watu wake!

Hata Yesu alionja adha kiasi cha wazazi wake kukimbilia uhamishoni, ushuhuda wa Fumbo la Maisha ya Kikristo! Kwa njia ya Wafranciskani wanaoendelea kutekeleza utume na shughuli zao za kichungaji nchini Siria, Kanisa linamwona Kristo Yesu anayeteseka! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa kinachomshirikisha mwamini katika historia ya kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Mashuhuda wa imani na wafiadini ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, hawa ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu; wamisionari wanaoendelea kupandikiza ukristo utakaochanua siku za usoni kwa njia damu yao!

Mashuhuda wa imani ni kielelezo cha utukufu wa Kanisa na chemchemi ya matumaini ya Wakristo. Ni kutokana na ukweli huu, mashuhuda wa imani na wafiadini wanaendelea kupambana na mawimbi mazito ya bahari katika maisha yao! Kumbe, ushuhuda huu unapaswa kuwa endelevu hata katika nyakati za shida na madhulumu, kwani kwa njia yao, watu wanapata wokovu. Bikira Maria aliweza kutekeleza dhamana na wajibu wake katika historia ya ukombozi kwa njia ya ukimya, akathubutu kusimama pale chini Msalabani, akamwangalia Mwanaye mpendwa, akiyamimina maisha yake, ili kutoa maana halisi ya maisha, yaani sadaka kwa ajili ya wokovu wa walimwengu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia Wafranciskani wanaotekeleza dhamana na wajibu wao nchini Siria kwamba, kila siku anawakumbuka katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na kwamba, hakuna jambo lolote lile linaloweza kuwatenganisha na upendo wa Kristo kama anavyofafanua Mtakatifu Paulo Mtume, kwani kila siku wanachungulia kaburi lakini bado wanaibuka washindi, kutokana na imani kwa Kristo Yesu anayewapenda upeo! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka Wafranciskani huko Siria chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aendelee kuwaombea neema ya udumifu!

Papa: Siria

 

 

28 November 2018, 11:10