Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kinyama Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kinyama Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati 

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kikatili Afrika ya Kati!

Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kumetokea mauaji ya watu zaidi ya 40 na kati yao kuna Mapadre wawili: Marehemu Padre Blaise Mada, Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Alindao pamoja na Padre Cèlestin Ngoumbango kutoka Parokia ya Kongbo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Novemba 2018, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliyaelekeza mawazo yake kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ambako kumetokea mauaji ya watu zaidi ya 40 na kati yao kuna Mapadre wawili: Marehemu Padre Blaise Mada, Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Alindao pamoja na Padre Cèlestin Ngoumbango kutoka Parokia ya Kongbo. Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati linasema, watu wengi wameuwawa kwa kuchomwa moto wangali hai, na Kikundi cha Seleka jambo la kusikitikisha sana.

Baba Mtakatifu anasema, amepokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa, kwa watu wasiokuwa na hatia waliokuwa wanapata hifadhi kwenye Kambi ya wakimbizi kuuwawa kikatili namna ile! Familia ya Mungu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, inayo nafasi ya pekee kabisa katika moyo wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye, aliitembelea na hatimaye kufungua Mlango wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaonesha upendo na uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala hasa wakati huu, wanapolilia amani ya kudumu.

Mashuhuda waliokuwa kwenye tukio wamesikitika kuona kwamba, Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa, “MINUSCA” vilivyoko nchini humo tangu mwaka 2014 havikuweza kuzuia mashambulizi haya ya kinyama. Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi na wahamiaji wapatao milioni 4. 5; watu wasiokuwa na makazi ya kudumu ni laki sita na tisini na kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanaopata hifadhi kutoka katika nchi jirani wamefikia laki tano na sabini elfu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati limeonesha masikitiko yake makubwa na linaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inawakamata wale wote waliohusika, ili waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria. Vikosi vya kigaidi nchini humo vimekuwa ni hatari sana kwa maisha na mali za wananchi. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipotembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati aliwakumbusha umuhimu wa kujenga na kukuza majadiliano ya kidini na kwamba, tofauti zao za kiimani, isiwe ni sababu ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Calfornia, waliokumbwa na janga la moto ambalo limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, hasara ya dola bilioni 2. 977 na kwamba, gharama za opresheni za zima moto ni zaidi ya dola bilioni 1, 366. Baba Mtakatifu amewakumbuka hata wale ambao wanateseka kwa baridi huko Mashariki wa Marekani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, apende kuwapokea kwenye nuru ya uso wake, wale wote waliofariki dunia kutokana na majanga haya asili ana kuwafariji wale wanaoteseka kwa sasa. Anawaombea watu wanaotoa huduma kuendelea kujisadaka ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kutokana na moto!

Papa: Maafa: CAR

 

 

18 November 2018, 10:55