Tafuta

Papa Francisko: Ukweli ni unyofu unaofumbatwa katika neno, tendo na uaminifu. Papa Francisko: Ukweli ni unyofu unaofumbatwa katika neno, tendo na uaminifu. 

Ukweli ni unyofu unaofumbatwa katika neno, tendo na uaminifu!

Ukweli ni ufunuo angavu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unaonesha Uso wa huruma na upendo usiokuwa na mipaka. Ukweli ni sehemu ya uwezo wa kufikiri ambao mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu lakini ni zawadi ya hali ya juu ambayo imemwilishwa katika Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu na wakweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanapaswa kuwa ni chumvi ya kuyakoleza malimwengu na mwanga wa kuyaangazia mataifa, ili yaweze kujikita katika utakatifu, kweli na haki na watu wanapoyaona matendo yao mema waweze kumtukuza Baba yao aliye mbinguni! Amri ya Nane inasema, “Usimshuhudie jirani yako uongo”. Huu ni mwaliko wa kuishi katika ukweli na hatimaye, waamini waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa kutekeleza nyajibu zinazoambatana na maisha yao! Amri ya Nane inakataza kupotosha ukweli katika mahusiano ya watu, kwani makosa dhidi ya ukweli yanaonekana kwa maneno na matendo. Ukweli uwasaidie waamini kukua na kukomaa katika upendo wa kidugu, haki na ujasiri kiasi hata cha kuungama imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 14 Novemba 2018 wakati wa Katekesi yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameendelea kuchambua Amri za Mungu na kwa wakati huu amefikia Amri ya Nane inajikita katika mawasiliano kati ya watu ndani ya jamii yanayopaswa kusimikwa katika ukweli, ili upendo uweze kung’ara na kushamiri. Wakati mwingine, ukimya unazungumza hata kuliko maneno na matendo, hali inayoonesha kwamba, daima mwanadamu yuko katika hija ya mawasiliano na kamwe hawezi kuishi bila kuwasiliana, hali inayowaweka katika makundi makuu mawili yaani: ukweli na uongo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukweli ni unyofu unaofumbatwa katika neno, tendo la kibinadamu na uaminifu. Ni tabia inayomwezesha mwanadamu kuwa mwaminifu katika maneno na mwangalifu dhidi ya kauleni, udanganyifu na unafiki. Uongo ni hatari sana katika mahusiano na mafungamano ya kijamii! Uongo unaua kwani ulimi una makali kuliko hata upanga, hali ambayo inawataka watu kuwa waangalifu na makini katika kutumia ndimi zao. Ulimi unaweza kumtumbukiza mtu katika vitendo vya kigaidi, vinavyoharibu sifa njema na utu wa watu wengine.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ukweli ni swali gumu ambalo Pilato alimswalisha Yesu wakati alipokuwa mbele yake, watu wakishuhudia uongo dhidi yake! Injili zinahitimisha simulizi la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, kwa Kristo mwenyewe kushuhudia kwamba, “Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli”. Ushuhuda wa Kristo Yesu unafumbatwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wake kutoka kwa wafu, ili kuwashirikisha walimwengu upendo wenye huruma wa Baba yake wa mbinguni, kielelezo makini cha uaminifu wake.

Waamini pia wamekirimiwa mapaji ya Roho Mtakatifu, Roho wa ukweli ambaye hushuhudia pamoja na roho zao kuwa wao ni watoto wa Mungu. Matendo na maneno ya binadamu yanaweza kukiri ukweli au kung’oa ukweli huu, wazazi na walezi waendelee kuwahimiza watoto wao kusema na kushuhudia ukweli. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa ni mashuhuda wa ukweli, kwani wao ni watoto wa Baba yao wa mbinguni ambaye kamwe hawezi kuwatelekeza, kwani anawakirimia upendo kwa ajili ya jirani zao, ukweli ambao unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha; kwa kufikiri, kusema na kutenda katika kweli.

Ukweli ni ufunuo angavu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unaonesha Uso wa huruma na upendo usiokuwa na mipaka. Ukweli ni sehemu ya uwezo wa kufikiri ambao mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu lakini ni zawadi ya hali ya juu ambayo imemwilishwa katika Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko kwa wafuasi wake kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili ya ukweli.

Baba Mtakatifu anahitimisha Katekesi yake kuhusu Amri ya Nane inavyosema “Usimshuhudie jirani yako uongo” kwa kukazia kwamba, mtu mkweli ni yule anayeishi kama mtoto mpendwa wa Mungu na hivyo kutoa nafasi kwa ukweli kuonekana, kwamba, Mungu ni ukweli na ndiye anayewakirimia imani katika yeye kwa kuwapenda, changamoto ya kujikita katika ukweli ili kuweza kushuhudia ukweli!

Papa: Katekesi
14 November 2018, 13:56