Ujumbe wa Papa Francisko & Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Haki Msingi za Binadamu miaka 70! Ujumbe wa Papa Francisko & Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Haki Msingi za Binadamu miaka 70! 

Kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Haki Msingi za binadamu!

Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 15-16 Novemba 2018 wanafanya kongamano la kimataifa linalojadili kuhusu: uhuru wa kidini, haki asilia, mabadiliko katika uhuru na utamaduni wa haki msingi za binadamu pamoja na upotoshaji wa dhana hizi katika Jumuiya ya Kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhuru wa kidini ni msingi wa: haki, utu na heshima ya binadamu! Jumuiya ya Kimataifa mwaka huu wa 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru mambo msingi yanayobainishwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu, ambalo, kwa Mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuchapishwa kwake!

Kuna umuhimu wa kukazia mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kama msingi wa kukuza na kudumisha amani duniani. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza! Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma, kuanzia tarehe 15-16 Novemba 2018 wanafanya kongamano la kimataifa linalojadili kuhusu: uhuru wa kidini, haki asilia, mabadiliko katika uhuru na utamaduni wa haki msingi za binadamu pamoja na upotoshwaji wa dhana hizi katika Jumuiya ya Kimataifa!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika ujumbe aliomwandikia Padre Federico Lombardi, SJ:,  Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, anawapongeza kwa kuchagua mada hizi kwani ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo, hasa kutokana na changamoto mamboleo ya kuibuka kwa haki msingi za binadamu, kuongezeka kwake na hatari ya baadhi ya haki hizi kuweza kutoweka kabisa. Mjadala huu ni muhimu sana katika mustakabali wa ulinzi na tunza ya familia ya binadamu, mjadala unaopaswa kupembuliwa kwa kina na mapana!  

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anapenda kuwahakikishia wawezeshaji na washiriki katika kongamano hili, uwepo wake kwa njia ya sala, ili Mwenyezi Mungu aweze kuibariki kazi ambayo ina thamani kubwa sana katika huduma ya Kanisa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote!

Kwa upande wake, Papa Francisko anasema, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbui kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipopitishwa na Umoja wa Mataifa, ni fursa si tu kwa ajili ya kuadhimisha tukio hili la kihistoria, lakini Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuzama zaidi kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Tamko la Haki Msingi za Binadamu mintarafu maendeleo ya Haki Msingi za Binadamu katika ulimwengu mamboleo. Juhudi za pamoja zinahitajika ili kubomolea mbali kuta za utengano zinazoivuruga familia ya binadamu, ili kuchochea mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Kumekuwepo na tafsiri tofauti kuhusu haki msingi za binadamu katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa, kiasi kwamba, zimeibuka “Haki Mpya” zinazosigana kati yake, kiasi cha kuibua matatizo makubwa kuhusiana na Haki Msingi za Binadamu. Hizi ni changamoto ambazo zilivaliwa njuga na Papa Mstaafu Benedikto XVI kama mwanazuoni mahiri na mchungaji, kiasi hata cha kustahili kupewa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Sheria, kutoka katika Chuo Kikuu cha LUMSA kinapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Hii itakuwa ni fursa ya kuweza kutafakari kwa kina na mapana mawazo ya Papa Mstaafu Benedikto XVI mintarafu haki msingi za binadamu, ili kulinda na kutetea utu na maendeleo fungamani ya binadamu.

Mfuko wa Ratzinger 2018
15 November 2018, 16:19