Tafuta

Kardinali Pasinya ang'atuka kutoka madarakani, Askofu mkuu Fridolin Besungu, ashika madaraka! Kardinali Pasinya ang'atuka kutoka madarakani, Askofu mkuu Fridolin Besungu, ashika madaraka! 

Kardinali Monsengwo ang'atuka; Askofu mkuu Besungu ashika usukani!

Baba Mtakatifu amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi mrithi Fridolin Ambongo Besungu, OFM, Cap. kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo kuu Katoliki la Kinshasa, nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi mrithi Fridolin Ambongo Besungu, OFM, Cap. kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo kuu Katoliki la Kinshasa, nchini DRC. Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu alizaliwa tarehe 24 Januari 1960.

Baada ya masomo na majiundo yake kitawa, kunako mwaka 1987 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1988. Baadaye aliendelea na masomo ya juu na hatimaye, kujipatia Shahada ya Uzamivu wa Taalimungu maadili kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsiana.

Tangu wakati huo, alibahatika kuwa Paroko usu tangu mwaka 1988 hadi mwaka 1989. Aliwahi kuwa Jaalim la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa; Mkuu wa Shirika na Makamu Mkuu wa Shirika nchini DRC. Amewahi pia kuwa Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Kitaifa nchini DRC, ASUMA na Mkuu wa Wakapuchini Barani Afrika, CONCAU. Akateuliwa na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bokungu-Ikela tarehe 6 Machi 2005.

Aliwahi pia kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Kole, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Aliwahi kuteuliwa kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Mbandaka-Bikoro kabla ya kuteuliwa na Papa Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo hilo. Tangu mwezi Juni 2016 amekuwa Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO.

01 November 2018, 15:46