Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania 

Kardinali Njue: Wosia kwa familia ya Mungu Tanzania kulinda imani

Katika mahubiri yake, Kardinali Njue alijikita zaidi katika wosia kwa makundi yanayounda familia ya Mungu nchini Tanzania, ili kila kundi liweze kuwajibika barabara katika kulinda, kutetea, kudumisha na kushuhudia imani katika matendo. Amelipongeza Kanisa nchini Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, nchini Kenya, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 4 Novemba 2018 amehitisha kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania, yaliyokuwa yanaongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji furaha ya Injili”. Hili ni tukio la kihistoria ambalo limehudhuriwa na familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania! Wachunguzi wa mambo wanasema,kwa hakika Bagamoyo mlango wa imani, pamenoga!

Katika mahubiri yake, Kardinali Njue alijikita zaidi katika wosia kwa makundi yanayounda familia ya Mungu nchini Tanzania, ili kila kundi liweze kuwajibika barabara katika kulinda, kutetea, kudumisha na kushuhudia imani katika matendo. Amelipongeza Kanisa nchini Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo na matunda yake yanaonekana. Akizungumzia kuhusu kundi la watoto, amewataka watoto kuwa wasikivu na watekelezaji wa mambo wanayoelekezwa na wazazi pamoja na walezi wao. Wazazi wamekumbushwa dhamana na wajibu wao wa malezi na makuzi kwa watoto wao na kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kurithishwa imani, maadili na utu wema!

Kardinali Njue amewakumbusha vijana kwamba, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unawaokodolea macho, ili kuwatumbukiza katika malimwengu na huko wasipokuwa makini, watakaiona cha mtema kuni! Imani, hekima, busara na dhamiri nyofu viwawezeshe vijana kutambua mema na kuyaambata na ubaya, kuufutilia mbali. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu analo lengo na makusudi kwa kila kijana, kumbe, ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, wanatambua na kuambata malengo ya Mungu katika maisha yao na kamwe wasibweteke na hivyo kumezwa na malimwengu!

Kardinali Njue akizungumza na wakleri, watawa na waamini walei na viongozi katika ujumla wao, amewataka kila mmoja wao, kuhakikisha kwamba, anatekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Waamini wajitahidi kutambua mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza. Kwa njia hii, wataweza kuenzi matunda ya kazi ya ukombozi. Wamisionari wa kwanza, hawakuangalia vikwazo, udhaifu na makando kando ya waafrika kwa wakati ule, wakajitosa bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa, kwa kukazia: utu, heshima na usawa mambo yanayovuka mipaka ya kibinadamu. Ukombozi wa kweli unafumbatwa katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Rais John Pombe Magufuli katika hotuba yake, ametoa shukrani za dhati kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania na kwamba, kama zilivyokuwa Serikali za awamu zilizotangulia, hata Serikali ya awamu ya tano itaendelea kushirikiana na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Tanzania, ili kukuza na kudumisha: ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Ameliomba Kanisa kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili aweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake. Amelitaka Kanisa lisaidie mchakato wa mapambano dhidi ya: rushwa na ufisadi; mmong’onyoko wa maadili unaojionesha katika vitendo vya ubakaji vinavyofanywa hata pengine na waamini.

Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji nchini Tanzania, anasema Rais Magufuli iwe ni fursa ya kuendelea kujikita katika: fadhila ya imani, upendo na mshikamano ili kukuza kanuni, maadili na utu wema, ili hatimaye, kuondokana na vitendo viovu vinavyochafua sura ya Tanzania. Amelishukuru Kanisa kwa mchango wake katika ustawi na maendeleo ya watanzania katika ujumla wao. Amesema, changamoto zinazolikabili Kanisa zitashughulikiwa kwa pamoja, ili Tanzania iweze kusonga mbele kwa upendo na mshikamano mkuu.

Watanzania wapende kumtanguliza Mungu katika maisha yao. Rais Magufuli amewaomba Maaskofu kumkumbuka na kumwombea katika utume wake kama Rais, anashangaa ni kwa kiasi gani watangulizi wake Mzee Jakaya Kikwete na Mzee Benjamin Mkapa walivyoweza kumaliza vipindi vyao vya miaka kumi ya uongozi. Rais Magufuli amesema, yeye pia ni tunda la uinjilishaji nchini Tanzania, aliwahi kwenda Seminarini, lakini kama yasemavyo Maandiko Matakatifu, wanaoitwa ni wengi, lakini wanaoteuliwa ni wachache, kumbe, yeye hakuteuliwa katika nafasi hiyo!

Kardinali Njue
05 November 2018, 10:21