Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sinodi iimarishe urika wa Maaskofu! Papa Francisko: Sinodi iimarishe urika wa Maaskofu! 

Papa Francisko: Sinodi iimarishe urika wa Maaskofu!

Baba Mtakatifu anasema, Sinodi ya Maaskofu ni kielelezo cha urika wa Maaskofu unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao msingi, ili kujenga na kuimarisha Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapendekezo kutoka kwa Mababa wa Sinodi yatakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na Barua ya Mababa wa Sinodi kwa Vijana Wote Duniani ni nyaraka kuu mbili zinazochota utajiri wake kutoka katika “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya kutendea kazi”. Baba Mtakatifu anasema, Sinodi ya Maaskofu ni kielelezo cha urika wa Maaskofu unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao msingi, ili kujenga na kuimarisha Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Mababa wa Sinodi wanaendelea kuhariri muswada wa mapendekezo ya Hati ya Mababa wa Sinodi utakaowasilishwa kwa Papa Francisko. Baada ya kusomwa, utapigiwa kura na hatimaye, Sinodi kufungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu, inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 28 Oktoba 2018. Katika kipindi hiki nyeti, Mababa wa Sinodi wanapaswa kuongozwa na Injili, Mapokeo ya Kanisa, Katekisimu ya Kanisa Katoliki na ukweli, ili kujibu: matatizo, changamoto na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya!

Mababa wa Sinodi wasikubali kutekwa na mawazo mepesi mepesi, ili kukumbatia mmong’onyoko wa maadili na utu wema; kwa kutaka kuwaridhisha baadhi ya watu. Maaskofu wanapaswa kusimamia, kutangaza na kushuhudia ukweli katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia bila kuyumbishwa kuhusiana na: tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Injili uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Wawe tayari kuendeleza utu, heshima na haki msingi za binadamu! Umoja na mshikamano ni mambo muhimu hata katika tofauti zao msingi.

Ndoa za watu wa jinsia moja, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni changamoto zinazohitaji: toba, wongofu wa kimisionari, sera na mikakati madhubuti ya shughuli za kichungaji. Wahusika washughulikiwe kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa na kwamba, Kanisa lijikite zaidi kushughulikia matatizo makubwa na changamoto nyingine, zitatuliwe kadiri ya busara ya kichungaji kwa Makanisa mahalia, bila kupokwa na ukoloni wa kisera!

Ikumbukwe kwamba, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ni changamoto iliyoibuliwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI, ikavaliwa njuga na viongozi wakuu wa Kanisa waliofuatia kama sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kutambua kwamba, Kanisa, kimsingi ni Sakramenti ya wokovu! Mtakatifu Paulo VI alitamani kuona kwamba, Urika wa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, unamsaidia katika dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Kanisa halina budi kuwaambata watu wote wa Mungu, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza, uongozi na karama za Roho Mtakatifu. Ni wajibu wa Maaskofu kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ili wote kwa pamoja waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee: “Urika wa Maaskofu” na “Dhana ya Sinodi” katika uongozi  kuanzia ndani ya Makanisa mahalia sanjari na uwajibikaji makini wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Mambo mengine ni uekumene na huruma kama mihimili mikuu ya kichungaji; uhuru wa kidini kwa mtu binafsi, watu wote na taasisi katika ujumla wake. Waamini walei walio wazi na wenye mwelekeo chanya; ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali hata katika utofauti wake ni kati ya mambo msingi yanayoweza kutekelezwa kwa dhati na Sheria za Kanisa kama chombo cha majiundo, ili kuwasaidia Wakristo kukua na kukomaa na hatimaye, kujisikia kuwa ni sehemu ya utamaduni unaojibu kwa dhati kabisa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican mintarafu “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na Urika wa Maaskofu.

Sinodi Vijana: Muswada
26 October 2018, 09:33